Mradi wa kuweka mashine mpya za kisasa za kukagua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ambazo zina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo mubashara kwenye mifumo ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) umekamilika.

Kukamilika kwa mradi huo kunatokana na maagizo aliyoyatoa Rais John Magufuli kuwa TPA na TRA zishirikiane kuendesha mashine za kukagua mizigo zinazotoa taarifa na picha mubashara, pamoja na kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha Serikali haipotezi mapato na kupitisha mizigo haramu.

Kuwepo kwa mashine hizo kutazisaidia TPA na TRA kubaini shehena zilizoko kwenye makasha yanayofikishwa bandarini hapo kupelekwa na kutoka nje ya nchi kama inawiana na nyaraka za mzigo huo; na hivyo kutozwa ushuru sahihi kwa mzigo stahiki. Lengo la kufunga mashine hizo ni kuongeza mapato kwa serikali.

Meneja wa Mradi huo, Zhang Sheng alisema jana kuwa mradi huo umekamilika na sasa wako katika hatua ya pili ya mafunzo na skana hiyo mpya inaweza kutumika muda wowote mara baada ya kukamilisha mafunzo.

Kwa mujibu wa Meneja huyo kutoka China, skana hiyo ina uwezo wa kusoma na kupeleka taarifa na picha za mizigo mubashara kwenye mifumo ya TPA na TRA kwa wakati mmoja bila kuchelewa. Kutokana na kukamilika kwa mradi huo, TRA na TPA zimeanza kuwapa mafunzo watumishi wao namna ya kutumia mashine hizo.

Jana Watumishi 20 wa mamlaka hizo kutoka Dar es Salaam na Tanga walihudhuria mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo ili wamudu kutumia skana hiyo inayotumia teknolojia ya kisasa.

“Nazipongeza Serikali za Tanzania na China kwa kuwezesha mradi huu kukamilika. Tunatarajia mafunzo hayo yatawaongeza uwezo wafanyakazi, ufanisi wa bandari pamoja na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko wakati akifungua mafunzo hayo ya siku tano.

Aliwaagiza washiriki kuhakikisha watakapokuwa wanafanya kazi katika mashine hizo wahakikishe wanafanya tathmini ya mizigo inayoonekana katika kontena kama ina taarifa sahihi kwa kulinganisha na nyaraka za kuagizia mizigo husika.

Pia aliwataka kuhakikisha nyara za Serikali, silaha haramu, dawa za kulevya, bidhaa za mionzi na nyingine zisizofaa hazipitishwi bandarini. Mkurugenzi huyo pia aliwataka watumishi hao kujifunza kufanya matengenezo ya mashine hizo angalau kwa asilimia 50 kuliko kutegemea wataalamu kutoka nje pekee.

Alisema TPA na TRA watahakikisha waendesha skana wanajifunza kufanya matengenezo kwa asilimia 100 ili kuondokana na gharama za kutumia wataalamu kutoka nje.

Wakati alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo, Rais alitoa miezi miwili kwa TPA kununua mashine nne za kisasa za kukagulia mizigo bandarini.

Alitoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni mashine mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwepo kwa udhibiti wa uhakika wa udanganyifu.

Awali baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waaminifu walikuwa wanatumia udhaifu wa mashine za bandarini hapo kusema uwongo kuhusu shehena inayokaguliwa bandarini hapo kwa lengo la kukwepa kulipa kodi stahiki.