Mbunge  wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameendelea kusota katika mahabusu ya Gereza la Kisongo mjini Arusha akiingiza siku ya 22 leo baada ya jana kukwama katika azma yake ya kutaka Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliomnyima dhamana.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi ndiye aliyetupilia mbali ombi la Lema, hivyo kumfanya arejee mahabusu huku mawakili wake wakihaha kuhakikisha wanakata rufaa ili kuomba dhamana hiyo katika ngazi nyingine ya kisheria.

Aidha, Jaji Moshi ameridhia ombi la Lema kupitia kwa mawakili wake Sheck Mfinanga na Peter Kibatala la kukata rufaa mahakamani hapo ili kesi hiyo isikilizwe na hatimaye Lema kupata dhamana baada ya kupitiwa na jaji atakayepangiwa.

Akitoa uamuzi huo mahakamani hapo, Jaji Moshi alisema kimsingi hoja ya mawakili wa Lema ya kutaka mahakama hiyo kuitisha faili na kulipitia haina msingi wowote kisheria hivyo anaitupilia mbali hoja hiyo na kutoa rai kwa mawakili hao kukata rufaa Mahakama ya Rufaa ili dhamana ya Lema isikilizwe.

“Mahakama hii haiwezi kupitia faili la kesi hii ya Lema ya kupata dhamana hivyo siwezi kupitia faili hili, bali nashauri mkate rufaa ili iweze kusikilizwa,” alisema Jaji Moshi.

Awali Wakili wa Serikali, Paul Kadushi aliwasilisha pingamizi Mahakama Kuu la kuitaka wasisikilize maombi ya Lema ya kutaka mahakama hiyo iitishe faili la kesi namba 440/441 kwa madai yapo makosa ya kisheria yaliyofanywa awali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa lengo la kumnyima dhamana mbunge huyo.

Akiwasilisha hoja zake mbele ya Jaji Moshi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Kadushi akisaidiana na Materu Marandu alisema anawasilisha hoja mbili za pingamizi za mahakama hiyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

Alisema kimsingi maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kutaka mahakama hiyo iitishe faili la kesi namba 440/441 yanakinzana na kifungu cha 43 (2) cha sheria ya Mahakama ya Mahakimu. Katika kesi hiyo, Lema anashitakiwa kwa kutoa maneno ya kumtusi Rais katika maeneo tofauti.

Kadushi alisema uamuzi unaopinga kufanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya kukubali kutompa dhamana Lema ni uamuzi mdogo na haukuwa na sababu za kukataa dhamana.

“Mahakama yako inafungwa mikono na kifungu hiki kufanya mapitio au uamuzi mdogo, hivyo tunaomba mahakama itupilie mbali maombi hayo,”alisema Kadushi ambaye wakati akiwasilisha hoja zake alikuwa akinukuu mashauri mbalimbali ya kesi zinazofanana na hiyo.

Aidha, Kadushi alisisitiza kuwa wao wanatambua haki ya kukata rufaa ipo wazi kwa mleta maombi ila itakuwa jambo geni kama mahakama itawapa nafasi kusikiliza maombi yao.

 Alisema hoja ya pili ya pingamizi lake, linatokana na mleta maombi kutokidhi matakwa ya kisheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Katika sheria ya makosa ya jinai, kifungu cha 359(1) ya mwaka 2002 kuwa mtu asiporidhika na maamuzi ya mahakama ya chini kama ilivyo katika kesi hiyo, kamwe hawezi kuwa na mbadala wa mapitio ya rufaa.

Akijibu hoja hizo Wakili anayemtetea Lema, Peter Kibatala akiwa na jopo la mawakili wenzake, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, John Mallya, Faraji Mangula na Charles Adiel, alipinga kuwekewa pingamizi hilo na kuomba mahakama isikilize maombi yao.

Alisema wao wamefungua maombi hayo kuiomba Mahakama Kuu kuitisha jalada la kesi ya mahakama ya chini ili kuona uhalali wa kutotekelezwa kwa uamuzi wa kutoa dhamana, kwani kilichokuwa kinasubiriwa ni masharti ya dhamana.

“Huyu mshitakiwa alipewa dhamana , ila kabla ya mahakama haijatoa masharti ya dhamana, upande wa serikali ukasimama kabla mahakama haijaweka masharti ya dhamana ambayo lazima ifanye hivyo, wakasema wameonesha nia ya kukata rufaa na mahakama ikakubaliana nao bila kutekeleza amri yao,” alisema Kibatala.

Aliomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi la serikali na kuiomba kuendelea na kazi iliyokusudia kuifanya ya kupitia maombi yao ili kutoa dhamana kwa mshtakiwa au iamuru mahakama ya chini kuendelea na uamuzi wake.

Wakili wa mbunge huyo baada ya maombi yao kugonga mwamba, walikuwa kwenye hekaheka ya kukamilisha kuandika rufaa ili kumnasua Lema atoke mahabusu.

Baada ya kutoka nje ya Mahakama Kuu, Wakili Mfinanga alisema wanamalizia kukamilisha taratibu za wao kukata rufaa Mahakama Kuu na wataomba rufaa hiyo isikilizwe kwa hati ya dharura ili kumnasua Lema mahabusu.