Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es-Salaam limetoa tahadhari kwa wakazi
wa kanda hiyo pamoja na wageni kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam
kwamba kuna baadhi ya matapeli wanatumia majina ya viongozi wa serikali
kujipatia fedha kinyume na sheria za nchi.
Kamishna
wa kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa
habari jana alisema kuwa jeshi hilo hivi karibuni limepokea malalamiko
kutoka kwa raia wa kigeni kuwa kuna wahalifu wanalitumia jina la Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuwataka watoe fedha kwa madai ya
kuwasaidia wanafunzi kupata vyuo nje ya nchi.
Alieleza
kuwa, mnamo Oktoba mosi mwaka huu raia wa china Marco Li mfanyakazi wa
kampuni ya Group six International alipigiwa simu na mtu
aliyejitambulisha kama Makonda na kumtaka atoe kiasi cha dola za
kimarekani 3500.
Alisema
tukio lingine lilitokea Oktoba 6, 2016 mkurugenzi wa kampuni hiyo
Jensen Huang aliitumia fursa hiyo kumwomba mkuu wa mkoa huyo bandia
kwamba amsaidie kumwidhinishia kuongezwa muda wake wa kuishi nchini
ambao ulikuwa umeisha, na kwamba mhalifu huyo alimtaka atoe dola za
kimarekani 7000 sawa na sh. Milioni 15.2.
Kamanda
Sirro amewataka wakazi wote wa Dar es Salaam na wageni kuwa makini na
matapeli hao na wakiona dalili za utapeli watoe taarifa katika vituo vya
polisi kwa msaada zaidi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
0 Comments
on