Raia watatu wa China wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kumteka na kumjeruhi raia mwenzao, Liu Hong.

Washitakiwa hao, Chen Chuw Bao (34), Wang Yong Jim (37) na Zheng Pa Jin (40) wamefikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai kuwa Oktoba 21, mwaka huu katika maeneo ya Palm Beach Ilala, Dar es Salaam Wachina hao walimteka raia mwenzao wa China, Liu Hong ili kumuweka kizuizini.

Alidai kuwa siku hiyo katika maeneo hayo ya Palm Beach, washitakiwa walimshambulia Hong katika sehemu za mwili na kusababisha apate maumivu ya misuli.

Baada ya kusomewa mashitaka Bao alikiri kutenda makosa yote, huku Jim akikiri kosa moja na Jin alikana mashitaka yote.

Wakili Moshi alidai kuwa amepokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam, SSP Salum Ndalama akiiomba Mahakama isitoe dhamana kwa washitakiwa hao.

Wakili Moshi alidai SSP Ndalama ametoa zuio hilo kwa kuwa washitakiwa hao ni raia wa China, pia hawana kazi wala hati za makazi ya kudumu.

Aidha, kuna taarifa za kuaminika kwamba washitakiwa hao na watuhumiwa wengine ambao hawajakamatwa wanapanga njama za kujihusisha na vitendo vya kihalifu ukiwemo utekaji.

Alidai washitakiwa hao na wengine ambao hawajakamatwa wana mpango wa kulipiza kisasi na endapo wakipata nafasi ya kupewa dhamana, wanaweza kwenda kupoteza ushahidi.

Wakili huyo, aliongeza kuwa rai ya SSP Ndalama ni kuwa, washtakiwa hao waendelee kubaki rumande hadi kesi hiyo itakapoisha ili kumlinda majeruhi pamoja na ushahidi. Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu.


==