Viongozi wa dini nchini waliopanga kumwona Rais John Magufuli kwa mazungumzo kuhusu hali ya siasa nchini wanaendelea kusubiri maombi yao kujibiwa licha ya kupita zaidi ya siku 90 sasa. 

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo  jana alisema: “Siwezi kusema Rais amekataa kuonana nasi, hapana. Labda ni kwa lile tulilokuwa tuende kumuona nalo (Ukuta) lakini kwa mazungumzo mengine milango ya Rais iko wazi,” alisema. 

Wazo la viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kutaka kuonana na Rais lilibuniwa Agosti ili kuzuia maafa ambayo yangejitokeza baada ya Chadema kutangaza kufanya maandamano waliyoyapa jina la Ukuta, Septemba Mosi. 

Hata hivyo, Dk Shoo alielekeza atafutwe Katibu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dk Leonard Mtaita kwa maelezo zaidi akisema ni mmoja wa wanaoratibu suala hilo. 

Dk Mtaita alipotafutwa kwa mara ya kwanza Septemba azungumzie kama barua waliyopeleka kwa Rais imejibiwa alisema tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera na kusababisha maafa makubwa litachelewesha mpango wao wa kukutana na Rais. 

Hata hivyo alipotafutwa tena jana, Dk Mtaita aliomba atafutwe mwenyekiti mwenza wa kikao kilichoibuka na wazo hilo ambaye ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim. 

“Tumewaachia wenzetu walioko Dar es Salaam, Sheikh Salim ndiye mwenyekiti mwenza na yeye yuko Dar na ndiye alijitolea kufanya mawasiliano na Mheshimiwa Rais,”alisema Dk Mtaita. 

Sheikh Salim alipotafutwa ili aeleze alipofikia kufanikisha kuonana na Rais alijibu kwa kifupi tu: “Sisi tuko katika kusubiri. Barua tulishatuma kwa Mheshimiwa Rais. Tunasubiri tu”. 

Msemaji wa Serikali, Hassan Abass alipoulizwa alitaka atafutwe Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kwa kuwa ndiye msemaji wa Rais. 

“Mtafute Msigwa maana yeye yupo karibu na Mheshimiwa (Rais Magufuli) na anajua ratiba zote,”alieleza. 

Alipotafutwa, Msigwa aliwataka viongozi hao kuendelea kusubiri kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake na pia inategemea ratiba ya Rais. 

“Kama wameandika, wasubiri watajibiwa,” alisema Msigwa.

Viongozi wa Chadema wanaposoma Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa wanaona wana haki ya kufanya mikutano ya ndani na hadhara na maandamano mradi tu Jeshi la Polisi litaarifiwe siku na mahali pa shughuli hiyo. 

Rais Magufuli alipiga marufuku siasa za ushindani hadi mwaka 2020 jambo ambalo Chadema waliamua kujitokeza kupinga kwa maandamano. 

Mbali ya Rais Magufuli, Jeshi la Polisi lilitangaza kuwa ni marufuku kufanya mikutano na maandamano. 

Hali hiyo iliyotishia kuwepo makabiliano yenye maafa ndiyo iliyowaibua viongozi wa dini ambao walichukua hatua kwanza kuwasihi viongozi wa Chadema na pili kuwataka wasubiri mrejesho