Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu tarehe 28 Novemba, 2016 wamekubaliana kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuboresha utendaji kazi wa reli ya TAZARA na bomba la mafuta la TAZAMA ili miradi hiyo miwili ilete manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi Tanzania na Zambia.
Marais hao wametangaza kuchukua hatua hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika muda mfupi baada viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 3 ya Rais Lungu iliyoanza jana hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Magufuli.
Katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya redio, tevisheni na mitandao ya kijamii Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na kuzorota kwa utendaji kazi wa reli ya TAZARA ambao umeshuka kutoka usafirishaji wa tani 5,000,000 za mizigo mwaka 1976 hadi kufikia usafirishaji wa tani 128,000 kwa mwaka hivi sasa, huku utendaji kazi wa bomba la mafuta la TAZAMA nao ukiporomoka kutoka uwezo wake wa kusafirisha tani 1,100,000 za mafuta hadi kufikia tani 600,000 kwa mwaka hivi sasa.
Marais hao wamekubaliana kuwakutanisha wanasheria wakuu wa Serikali za nchi zote mbili haraka iwezekanavyo kwa lengo la kufanya marekebisho ya kisheria kwa maeneo yote yaliyoonesha kuwa kikwazo na pia kupanga upya menejimenti za TAZARA na TAZAMA ili ziweze kuendesha vyombo hivyo kibiashara na kwa manufaa yaliyokusudiwa wakati vilipoanzishwa na Waasisi wa mataifa haya mawili yaani Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mhe. Dkt. Kenneth Kaunda wa Zambia.
“Tumekubaliana ni lazima tubadilike na tubadilike kwa haraka, vikwazo vinavyotokana na sheria viondolewe na manejimenti ya TAZARA ipangwe upya, na mimi nataka kusema kwa uwazi, ukiwauliza TAZARA watakwambia tatizo ni mtaji lakini ukweli ni kwamba tatizo ni menejimenti, ingekuwa tatizo ni mtaji, ule uliokuwepo mwaka 1976 umekwenda wapi? maana sasa hivi TAZARA ina vichwa 14 tu vya kuendeshea treni na ina upungufu mkubwa wa mabehewa” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Lungu amesisitiza kuwa katika kuimarisha TAZARA wamekubaliana kuweka pembeni siasa na kuirejesha TAZARA katika hali yake ya kibiashara kwa kuhakikisha inafanya kazi ya kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo iendayo kusini mwa Tanzania na nchini Zambia.
Mhe. Lungu ameongeza kuwa pamoja na kuimarisha bomba la mafuta la TAZAMA, Zambia inatarajia kunufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania na pia inajipanga kutumia vizuri fursa ya kufunguka kwa ukanda wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Corridor) na mpango wa ujenzi wa reli ya kati ambapo ukanda wa Kaskazini mwa Zambia una mawasiliano ya karibu na bonde la ziwa Tanganyika.
“Mhe. Rais Magufuli una muda wa kutosha katika uongozi wako na mimi nina muda wa kutosha pia, kwa hiyo kwa pamoja tunaweza kuimarisha maeneo yote ya kuinua biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili ikiwemo kuimarisha TAZARA na TAZAMA kwa manufaa ya wananchi wetu” amesisitiza Rais Lungu.
Kuhusu hali ya biashara kati ya Tanzania na Zambia, Rais Magufuli amesema Zambia ni nchi inayoongoza kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam ambapo katika mwaka 2015 mizigo yenye uzito wa tani Milioni 1.9 ilipitishwa na kwamba kumekuwa na ongezeko la biashara kati ya Zambia na Tanzania kutoka Shilingi Bilioni 89.2 mwaka 2010 hadi kufikia Shilingi Bilioni 152.2 mwaka 2015.
Dkt. Magufuli amemhakikishia Rais Lungu kuwa Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ikiwa ni pamoja na kuboresha zaidi bandari ya Dar es Salaam, kupunguza vizuizi vya barabarani kutoka 8 hadi 4, kushughulikia tatizo la vizuizi vya polisi na kujenga Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post)
“Tunataka mambo haya yote yaende haraka, wataalamu wetu ni lazima waharakishe kurekebisha vikwazo vyote vilivyokuwa vinatuchelewa, tufanye kazi pamoja kwa manufaa ya wananchi” amesisitiza Rais Magufuli.
Jioni ya leo Rais Edgar Chagwa Lungu anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam na kesho Rais Lungu anatarajiwa kumaliza ziara yake ya siku 3 hapa nchini.
0 Comments
on