Leo ni mapumziko ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambapo Waislamu nchini wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha siku hii muhimu katika imani ya dini ya Kiislamu.
Maulid ilisomwa usiku wa jana kuamkia leo na leo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid.Maadhimisho ya Maulid kitaifa yanafanyika mkoani Singida.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Singida, Alhaji Buruhani Mlau alisema jana kuwa maandalizi yako vizuri na kuwataka waumini wa dini hiyo kuwa watulivu na kusherehekea kwa amani.
Awali Alhaji Mlau alisema sherehe hizo za Kitaifa za Maulid zinafanyika katika kijiji cha Shelui, wilayani Iramba, mkoani hapa na kwa utaratibu sherehe hii mapumziko ni siku moja.
Wiki iliyopita, akitangaza utaratibu wa sherehe hizo, Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir alisema kwa mwaka huu, Maulid itasomwa usiku wa Desemba 11 na mapumziko yatakuwa siku inayofuata yaani Desemba 12.
Mufti wa Tanzania aliwataka Waislamu wote nchini waadhimishe Siku ya Maulid kwa kufanya usafi, kupanda miti na kuchangia damu.
“Waislamu wanatakiwa kutumia siku hiyo kwa kufanya matendo mema na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kufanya usafi kwenye mitaa yao na kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji huo,”alisema Mufti.
0 Comments
on