Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa wiki tatu sasa haitoi huduma ya ubadilishaji noti chakavu na sarafu hivyo kuwasababishia wananchi usumbufu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliofika BoT kubadilisha fedha hizo walisema taarifa za kurejeshwa huduma hiyo zimekuwa zikibadilika siku hadi siku.

“Nilipokwenda kubadilisha noti nilikuta tangazo kwenye lango la kuingia benki lililosema huduma ya ubadilishaji noti chakavu imesitishwa kwa muda na itaanza Novemba 28,” alisema mkazi wa mjini hapa, Joel Mwakasege .

Alisema alipokwenda Novemba 28, alikuta tangazo limebadilika na kuonyesha huduma itarejeshwa Desemba 5. “Ni usumbufu, watu wanatoka mbali kuja kubadilisha sarafu na noti lakini hawaelezwi ukweli ni lini huduma itarejeshwa.”

Meneja Uhusiano wa BoT, Zalia Mbeo alisema ilisitishwa kwa muda kwa kuwa watoa huduma hiyo walitingwa na majukumu mengine muhimu na kuanzia keshokutwa itafanyika kama kawaida.

Mkazi wa Tegeta, Israel Mwinyimvua alisema tatizo siyo kusitishwa kwa huduma hiyo bali matangazo kubadilika.

“Tunaomba siku nyingine wawe na uhakika wa matangazo wanayotoa kwa kuwa wanawasabishia usumbufu wananchi,” alisema.

Alisema zamani benki za biashara zilikuwa zikibadilisha noti chakavu lakini hivi sasa huzikataa na sehemu pekee ya kufanya hivyo ni BoT.