Header Ads Widget

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA Harry Kitilya na Wenzake wafungua kesi ya kikatiba Wakupinga Kunyimwa Dhamana

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake
watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya utakatishaji
fedha katika kesi mbili tofauti wamefungua kesi ya
kikatiba wakipinga kunyimwa dhamana.
Kitilya, Shose Sinare na Sioi Solomon,
wanaoshtakiwa katika kesi moja na nyingine ya
utakatishaji fedha inayomjumuisha, Gidion
Wasongo wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu.
Mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wa pili ni
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa
Mashtaka ( DPP).
Kesi hiyo ya kikatiba namba 14 ya mwaka 2016,
Kitilya na wenzake wanapinga kifungu cha 148 (5)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
(CPA), kinachozuia dhamana kwa mashtaka ya
utakatishaji fedha.
Wanadai kuwa kifungu hicho kinakiuka Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka
1977, Ibara ya 13 (b).
Ibara hiyo inazuia mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la
jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo
mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya
kutenda kosa hilo.
Pia, wanadai uamuzi wa kuwafungulia shtaka la
utakatishaji fedha haukuwa wa haki, bali ulikuwa
na nia mbaya ya kuwanyima dhamana.
Kesi hiyo imepangwa kuanza kutajwa leo
mahakamani hapo, kabla ya kuendelea na taratibu
nyingine za usikilizwaji wa hoja za msingi za
wadai hao.
Wakati Kitilya, Sinare na Sioi wakikabiliwa na
shtaka hilo katika kesi moja, Wasongo anakabiliwa
na shtaka hilo katika kesi tofauti yeye na wenzake
wengine akiwamo aliyekuwa Mhasibu wa TRA,
Justice Katiti.
Hata hivyo, licha ya kesi hiyo ya kikatiba,
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga
kutoa uamuzi wa rufaa dhidi yao Agosti 9, ambayo
DPP anapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wa kuwafutia shtaka la utakatishaji
fedha.
Katika kesi ya msingi, Kitilya na wenzake
wanakabiliwa na mashtaka manne ya kughushi,
kuwasilisha nyaraka za uongo, kujipatia fedha Dola
za Marekani 6 milioni kwa njia za udanganyifu na
kutakatisha fedha kiasi hicho, ambalo liliwafanya
wakose dhamana.
Hata hivyo, ilikuwa ni furaha kwao baada ya
Mahakama hiyo baadaye kuwafutia shtaka hilo,
kutokana na juhudi za mawakili wao, Dk Ringo
Tenga, Majura Magafu na Alex Mgongolwa
kulipinga kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria
kuitwa kosa la utakatishaji fedha.
Lakini DPP hakukubaliana na uamuzi huo wa
Mahakama ya Kisutu, hivyo alikata rufaa
Mahakama Kuu, lakini Mahakama Kuu katika
uamuzi uliotolewa na Jaji Moses Mzuna ilitupilia
mbali rufaa hiyo pamoja na mambo mengine
akieleza kuwa hapakuwa na haja kukata rufaa kwa
uamuzi huo.
DPP hakukubaliana pia na uamuzi huo wa
Mahakama Kuu, hivyo alikata rufaa Mahakama ya
Rufani na akashinda na mahakama hiyo iliamuru
Mahakama Kuu isikilize upya rufaa ya DPP.

Post a Comment

0 Comments