Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amepiga
marufuku mikutano ya Operesheni Ukuta
iliyotangazwa kuratibiwa na Chadema kuanzia
Septemba Mosi.
Akizungumza katika kikao cha kazi
kilichoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama mkoa,
wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa
halmashauri, Makalla alitangaza kupiga marufuku
mkutano wowote utakaofanyika chini ya utaratibu
unaoitwa Operesheni Ukuta.
“Bila shaka wananchi wa Mbeya wanataka amani
na kazi, hivyo ni marufuku kufanyika mkutano
wowote wa kisiasa unaoandaliwa kwa kushirikiana
na watu wengine kutoka nje ya mkoa,” alisema
Makalla aliyewahi kuwa mbunge na mweka hazina
wa CCM.
Alifafanua kuwa wabunge na madiwani akiwamo
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu)
wa Chadema wanaweza kufanya mikutano yao bila
wasiwasi katika maeneo yao.
Makalla alisema vyombo vimewekwa tayari
kuwashughulikia kwa nguvu zote watakaokaidi
maagizo yanayotolewa na kutoa mwito kwa vijana
wa mkoa huo kuwafichua watu wenye njama
zozote zikiwamo za kuwahamasisha kufanya
maandamano au mikutano.
Polisi yadai kukamata vijana
Wakati Makalla akipiga marufuku Operesheni
Ukuta, Polisi mkoani Mbeya wameeleza
kuwakamata vijana wawili wanaodaiwa kuwa
wafuasi wa Chadema kwa tuhuma za kuandaa na
kusambaza ujumbe wa sauti wenye kauli za kutaka
ofisi za CCM zichomwe moto.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Dhahir
Kidavashari alidai kwamba vijana hao waliandaa na
kusambaza ujumbe huo Julai 29 ukiwataka vijana
wenzao ambao ni wanachama wa chama hicho
kwenda kuchoma moto ofisi za CCM mahali
walipo.
Kidavashari alidai kwamba ujumbe huo
unahamasisha vijana kufanya uhalifu huo wakati
wowote kabla ya Septemba Mosi na baada ya
hapo ilimradi nchi iwe kwenye machafuko.
“Baada ya kufuatiliwa na kumkamata, mtuhumiwa
wa kwanza alipekuliwa na kukutwa na simu ambazo
zilitumika kusambaza ujumbe huo.Pia kupitia
mtuhumiwa huyo tulifanikiwa kumpata mtuhumiwa
mwingine.