Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu amekamatwa na polisi muda mfupi baada ya
kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo
wa Ikungi, Singida.
Wakati Lissu akiwa mikononi mwa polisi, Mbunge
wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa jana
alifanya mkutano wa hadhara na kusema hakuna
wa kumpangia cha kuzungumza kwenye mikutano
yake.
Kukamatwa kwa Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa
Chadema ndiye aliyetoa taarifa za kukamatwa
kwake kwenye mtandao akisema: “Wakubwa sana
salaam. Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini
ya ulinzi wa polisi Singida.
" Nimemaliza kuhutubia mkutano wa hadhara mji
mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya Jimbo
langu la Singida Mashariki. Mara baada ya kushuka
jukwaani nimefuatwa Regional Crimes Officer (RCO)
wa Mkoa wa Singida aliyejitambulisha kwa jina la
Babu Mollel na kunitaarifu kuwa ameelekezwa na
Regional Police Commander (RPC) Singida
nikamatwe apparently (dhahiri) kuna amri ya
kunikamata iliyotoka Dar es Salaam.
“Kwa hiyo niko nguvuni na ninasubiri maelekezo ya
RPC juu ya wanakotakiwa kunipeleka. It’s likely
(inawezekana) nitasafirishwa Dar usiku huu. In fact
(hakika) ni usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa
vyovyote itakavyokuwa, there’s no turning back.
There’s no shutting up (hakuna kurudi nyuma,
hakuna kunyamaza).
"Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema
watawala popote nitakapokuwa, whether in freedom
or in jail (niwe huru au jela)... Aluta continua!. "
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias
Sedoyeka alithibitisha kukamatwa kwa Lissu
lakini alikataa kutoa sababu za hatua hiyo.
Chadema jana jioni ilitoa taarifa kuhusiana na
kukamatwa kwa Lissu ikisema: “Tunaweza
kuthibitisha kwa vyombo vya habari kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Chama Mh. Tundu Lissu
anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida kwa
sababu ambazo hazijawekwa wazi.”
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa
Chadema, Tumaini Makene ilibainisha kuwa Polisi
walimkamata jana jioni baada ya kumaliza
mkutano wake wa hadhara alioufanya Ikungi
jimboni kwake na kueleza kuwa viongozi wa
chama hicho mkoani humo walikuwa polisi
kuhakikisha anapata haki zake kama inavyostahili
na kwamba ofisi ya katibu mkuu inafuatilia kwa
ukaribu kujua sababu hasa ya kushikiliwa kwake na
kutoa msaada wa haraka kadri itakavyohitajika.
Lissu amekuwa kwenye misukosuko na Jeshi la
Polisi mara kadhaa na kwa siku za karibuni
alikamatwa na kufikishwa mahakamani
akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kwenye
gazeti la Mawio.
Sambamba na kesi hiyo, Lissu alikamatwa na
polisi kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi
baada ya kupata dhamana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
Msimamo wa Msigwa
Mkoani Iringa, Msigwa akizungumza kwenye
mkutano wa hadhara wa kwanza wa kibunge tangu
alipochaguliwa uliofanyika kwenye viwanja vya
Mwembetogwa mjini hapa, alisema hakuna wa
kumpangia hoja za kuzungumza kwenye mikutano
yake.
Juzi, mbunge huyo alipewa barua na Jeshi la
Polisi iliyoeleza kuwa imempa kibali cha kufanya
mikutano hiyo, lakini ikimuwekea masharti
mbalimbali likiwamo la kutozungumzia viongozi
wengine na badala yake ajikite kwenye shughuli za
maendeleo na kuchukua maoni ya wananchi
anaowawakilisha.
Pia, alitakiwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu kutoka
nje ya Mkoa wa Iringa au eneo lolote lililo nje ya
mamlaka atakayeruhusiwa kuzungumza.
Lakini jana akihutubia alisema: “Ninaona watu
wote mna nyuso za hofu na mimi nimekuja
kuwaondoa hofu …hakuna mtu mwenye mamlaka ya
kunipangia cha kuzungumza, sipo hapa kwa
matakwa ya polisi … mimi nipo kwa matakwa ya
kisheria na ninazungumza kwa mamlaka
mliyonipatia.
“Pia Katiba inaeleza wazi mad raka na kinga ya
Mbunge… mbunge anayo haki ya kuitisha na
kufanya mkutano wa hadhara kwa mjibu wa
sheria.”
Kuhusu Rais kuzuia mikutano ya vyama vya siasa,
Msigwa alisema hakubaliani na hatua hiyo kwa
madai kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa Katiba ya
nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka
1992 ambavyo nchi inayoongozwa chini ya utawala
wa kidemokrasia inapaswa kuvifuata.
“Ninamuunga mkono na ninampongeza Rais John
Magufuli kwa kupambana na ufisadi, anapinga
rushwa… lakini siungani naye kwa kitendo chake
cha kukandamiza demokrasia nchini na niwaombe
wananchi wa Iringa kuungana na mimi kumpinga
mtu anayekandamiza demokrasia nchini,” alisema.
Kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, mbunge huyo
ambaye pia ni waziri kivuli wa Wizara ya Mambo
ya Nje, alikosoa uamuzi huo akisema hajawahi
kuona katika mipango yote iliyowasilishwa na
Serikali bungeni inayoelekeza hilo.
“Serikali ilileta mpango wake wa miaka mitano,
mwaka mmoja na Bajeti, hivi vyote vinaletwa
bungeni na baada ya kujadiliwa na kupitishwa,
vinatungiwa sheria ili viweze kutekelezwa hivyo
vipaumbele vyake ni lazima vifiti kwenye mipango
hiyo,” alisema Msigwa na kuongeza:
“Lakini katika vyote vitatu vya mwaka huu, mpango
wa miaka mitano, mwaka mmoja na hata katika
bajeti ya mwaka huu sijaona mahali popote
palipoandikwa kipaumbele cha Serikali ni kuhamia
Dodoma.”
Msigwa alisema kuhamisha Serikali ni gharama
kubwa na kuwataka wakazi wa Iringa na maeneo
mengine kuhoji suala hilo kama ndicho
kipaumbele cha maendeleo na mahitaji yao.
Alisema wamejipanga kufanya shughuli za
maendeleo ikiwamo miradi ya barabara, kuboresha
huduma za afya, usafi wa mazingira na
miundombinu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa
halmashauri hiyo wakiongozwa na Mstahiki Meya,
Alex Kimbe.
0 Comments
on