Header Ads Widget

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 26

MTUNZI: ENEA FAIDY
....BI CAROLINA alipiga hatua za taratibu kuelekea
sebuleni lakini hali iliyokuwemo ndani mle ilizidi
kumshangaza kwani alisikia harufu Kali na mbaya
ya kitu kuungulia. Alifika sebuleni lakini hakukuta
Mtu yeyote, akaamua kwenda jikoni.
Alipoingia jikoni tu, alipiga chafya tatu mfululizo
kutokana na moshi mzito ulioambatana na harufu
Kali sana uliotawala jikoni mle. Aliisogelea mpaka
sehemu ya kupikia akagundua moto uliwashwa na
kuna kitu kilichomwa. Akaangalia sufuria zote
lakini hakukuta kitu chochote, akabaki na
mshangao.
"Doreen!" Aliita Bi Carolina akiwa ameshika mkono
kiunoni.
"Abee mama!" Sauti ya Doreen ilisikika kutoka
chumbani.
"Njoo huku jikoni"
Bila ya kuchelewa Doreen alifika jikoni kule na
kumkuta Bi Carolina akiwa ameshika kiuno
akimsubiri kwa hamu amuulize kilichotokea.
"Abee mama" aliitikia Doreen kwa adabu sana.
"Nini kimetokea huku jikoni?"
"Nisamehe mama... Nilitaka kupika.. Ila kwa
bahati mbaya nikaunguza kwani sijui kutumia jiko
la gesi." Alijitetea Doreen huku akitia huruma sana.
"Ulitaka upike nini asubuhi yote hii?"
"Nili...nilikuta maziwa.. Nyama kwenye friji
nikataka nipike.."
"Mara maziwa mara nyama.. Mbona sikuelewi?
Haya ulipikia sufuria gani?" Bi Carolina alishindwa
kumuelewa Doreen ila kutokana na ugeni aliokuwa
nao hakuweza kumfokea sana kwa kuhofu kuwa
atajisikia vibaya.
"Nilichukua nyama... Sufuria ilipoungua sana
nikaamua kuiosha.." Alisema Doreen akidai
kutetemeka kwa woga.
"Sawa ila usirudie tena.. Nitakufundisha jinsi ya
kupikia jiko la gesi.."
"Sawa mama" alisema Doreen kwa sauti ya upole
iliyojaa hekima ya viwango vya juu.
"Sawa mwanangu nenda kaendelee na kazi zako"
Doreen alitoka jikoni mle na kuelekea chumbani
kwake. Alichukua kimfuko cheusi kidogodogo
kisha akafungua na kuutoa ungaunga mweusi.
Kisha akaweka kiganjani na kusogelea kila kona ya
chumba kile na kuupuliza kwa midomo yake.
Alifanya hivyo mpaka unga ule ilipoisha,
akasogelea kitanda chake na kukaa.
"Hapa sasa nimemaliza kazi... Mpaka huo moshi
uishe nitakuwa nimefanikiwa kabisa." Alisema
Doreen akitabasamu kwani ule moshi uliotapakaa
ndani mle ulisababishwa na Doreen. Alikuwa
amechoma dawa ambayo ingewafanya wakaaji wa
nyumba ile kumpenda Doreen kupita kiasi, na
wasingeweza kumfukuza hata iweje mpaka pale
atakapoamua kuondoka yeye mwenyewe.
Aliangalia SAA yake ya mkononi ilikuwa tayari ni
saa nne na nusu asubuhi. Doreen alisikia sauti ya
Bi Carolina ikimwita. Akatii wito na kumfuata Bi
Carolina.
"Abee mama" aliitikia kwa heshima.
"Umeoga?"
"Bado"
"Kaoge unywe chai."
"Sawa mama"
Doreen alitoka sebuleni pale na kwenda bafuni
kuoga. Alipomaliza alipaka mafuta na kuvaa tena
nguo alizokuwa amevaa kabla ya kuoga kisha
akaenda sebuleni. Akamkuta Bi Carolina akiwa
amekaa huku akitazama televisheni.
"Mbona umevaa nguo chafu?"
"Sina zingine"
"OK.. Baadae tutaenda Mwanjelwa ukatafute nguo
za kuvaa.. Sasa hivi nenda ukanywe chai.."
Alisema Bi Carolina.
"Sawa mama.. Vipi kuhusu Dada Pamela?" Aliuliza
Doreen.
"Atakuja si muda mrefu.. Ameniambia yupo njiani.
Baada ya kumwambia hivyo ghafla mlango
ukagongwa . Akaingia msichana mmoja mrefu
kiasi, mweupe, matiti yenye ukubwa kiasi, kiuno
chembamba kama sindano na makalio makubwa
kama milima miwili iliyopangana vyema. Wote
walishtuka kidogo.
"Ah Pamela kumbr ulikuwa jirani tu..
Tumekuongelea sasa hivi hapa.."
"Sikuwa mbali"
"Karibu sana" alisema Bi Carolina wakati huo
Pamela alikuwa akiketi sofani na kuweka pembeni
mkoba wake. Kwa muda wote huo Doreen alikuwa
akimtazama Pamela katika maeneo ya kifuani.
"Shkamoo Dada Pamela" alisalimia Doreen
"Marhaba hujambo? Wewe ndo Doreen?"
"Ndio.." Aliitikia Doreen huku akimgeukia mama
Pamela "kumbe una mtoto mzuri namna hii?"
Alisema.
Bi Carolina na Pamela walicheka tu.
"Huyu ndo mwanangu mpenzi... Yuko peke yake
kama Tanzanite..." Alisema Mama Pamela huku
akicheka.
Doreen aliwaacha wakiendelea na mazungumzo
kisha yeye akaenda chumba cha kulia chakula
(dinning). Moyoni mwake alifurahi sana kwani kwa
uzuri aliokuwa nao Pamela titi lake lilifaa sana kwa
kazi ya Doreen.
********
Dorice aliitazama Pete ya Mansoor kwa mshangao
kwani hakujua lengo kamili la Mansoor kutaka
kuitazama Pete ile.
"Umeitazama vizuri Pete hiyo?"
"Ndio"
"Hii Pete, si kama Pete za kawaida, ina nguvu
nyingi sana ambayo inazidi nguvu za kaeaida."
Alisema Mansoor kisha akakohoa kidogo ili
kusafisha koo lake kisha akaendelea.
"Pete hii nilipewa na babu yangu ambaye anaishi
mbali sana katika sayari nyingine kabisa, alinipa
kwaajili ya ulinzi wangu binafsi kwasababu alikuwa
ananipenda. Na Mimi nitakupa wewe pete hii
kwasababu nakupenda sana, ili ikusaidie katika
kumuokoa mtu umpendae sana." Alisema Mansoor
huku akimtazama Dorice. Dorice aliendelelea
kumsikiliza kwa umakini sana Mansoor.
"Pete hii ni ya ufalme wangu pale nitakapopewa
ufalme na mama yangu... Wewe kwasababu ni
mke wangu utakuwa malkia..."
"Nini?"
"Unashangaa nini? Sina njia nyingine ya kukusaidia
mbali na hii.. Kama upon tayari nitakupa pete hii
na utakuwa na uwezo mkubwa sana wa kijini...
Utarudi duniani na utafanya kila unalotaka..."
Alisema Mansoor. Maneno yake yalikuwa mazuri
masikoni mwa Dorice ingawa yalimpa utata wa
kiwango cha juu alijiuliza maswali mengi kichwani
mwake juu ya suala la umalkia. Lakini
akayapotezea maswali yake kwani alitamani sana
kurudi duniani kumuokoa mpenzi wake Eddy na
kwenda kwa wazazi wake ambao hakuwaona kwa
muda mrefu.
"Sawa... Nipe tu..!" Alisema Dorice akionesha
kukubali masharti ya Mansoor.
"Nitakupa Mke wangu lakini kuna jambo muhimu
unalotakiwa kuzingatia pindi utakapokuwa na hii
pete"
"Jambo Gani?" Dorice alishtuka.
"Hii ni pete ys heshma sana, ambayo haihitaju
uchafu wa aina yoyote.. Kwahiyo ukiivaa na
kwenda Nayo duniani hutakiwi kufanya mapenzi na
mwanaume mwingine zaidi yangu Mimi!" Alisema
Mansoor huku akimtazama mkewe kwa macho
yaliyoonesha msisitizo kwa kile alichokizungumza.
"Mmh!" Aliguna Dorice kwani alikuwa na wazo la
kumsaliti Mansoor pindi atakaporudi duniani. Na
alikuwa na lengo la kutorudi tena katika himaya ile
ya majini. Hivyo basi masharti ya pete ile yalikuwa
magumu sana kwake na kumuweka katika wakati
mgumu sana.
"Mbona unaguna?"
"Kwani hakuna msaada mwingine mbali na hiyo
pete" aliuliza Doreen
"Upo!"
"UPI.. Nipe msaada mwingine Mansoor tafadhali"
"Unataka njia nyingine?"
"Ndio.." Alijibu Dorice haraka.
**********
Mr Aloyce alitembeatembea katika eneo lile
akimsubiri mkewe atokeze lakini muda ukazidi
kwenda Vila kuona dalili yoyote. Mr Aloyce alianza
kukata tamaa ya kumpata mkewe akahisi huenda
alikuwa anadanganywa tu. Akataka kuondoka lakini
moyo wake ulisita sana baada ya kuumbuka
msemo usemao "atafutaye hachoki, akichoka
keshapata" akaamua kuwa mvumilivu kwani siku
zote mvumilivu hula mbivu.
Ajasogelea eneo tulivu lenye nyasi fupi kisha
akaketi pale. Mawazo mengi yalifurika kichwani
mwake, "nimekuwa mtumwa... Mtumwa wa nguvu
za giza hii hali mpaka lini? Kila siku yanaibuka
mapya... Mmh! Yote hii ni kwasababu ya Eddy..
Ila sipaswi kumlaumu" alijiwazia Mr Alloyce huku
machozi yakimtiririka.
Ghafla upepo mkali ulianza kupuliza eneo lile na
kumwondoa mawazoni Mr Aloyce. Alinyanyuka
pale chini na kutazama juu lakini hakuona
chochote.
Upepo ukazidi kupuliza kwa kasi sana mpaka miti
ikaanza kuyumbayumba. Miti iliyumba kwa kasi
sana na ile isiyo na nguvu ikaanguka. Mr Aloyce
aliogopa sana.
Baada ya upepo ule radi Kali zikapiga mfululizo,
zikazidi kumtisha Mr Aloyce. Alipiga hatua
kuelekea kwenye gari yake ili akajifiche mle maana
hali ilitishs lakini ghafla akasikia sauti ya kilio
kikali.
"Nisaidie mume wangu.. Nisaidiee!" Mr Aloyce
alishtuka sana kwani sauti ile aliijua fika. Ilikuwa ni
sauti ya mkewe mpenzi. Akabaki amesimama
wima kama mlingoti ili asubiri kitakachoendelea.
Akiwa bado amesimama alishtushwa na kitu
kikipita miguuni mwake, akatulia kimya huku
akipiga jicho kutazama kilikuwa kitu gani.
"Mamaaa" mr Aloyce alipiga ukunga kwa woga na
hofu baada ya kuonana uso kwa uso na chatu
aliyekuwa akijiviringa kwa kasi mwilini mwake.
Itaendelea.....

Post a Comment

0 Comments