WATU wanaosadikiwa kuwa ni polisi mkoani Shinyanga wanadaiwa kuanzisha vurugu baada ya kuagiza chipsi na kukataa kuzilipa, kisha kuanza kuwapiga wauzaji na kuwabambikizia kesi.

Tukio hilo linaelezwa kuwa lilitokea hivi karibuni katika eneo la Mshikamano, kata ya Ngokolo, katika Manispaa ya Shinyanga majira ya usiku, wakati askari hao wakidaiwa kwenda kwa muuza chipsi kwa ajili ya kununua.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Salumu Saidi ambaye ni muuza chipsi aliyedai kufanyiwa vurugu, alisema askari hao walikuwa zaidi ya wanne, lakini wawili ndio walioomba wakaangiwe chipsi.

“Wakati naweka chipsi katika chombo cha kukaangia walianza kula kabla ya kuiva na nilipotaka kuweka mayai waliniambia niongeze kwa madai kuwa ni ndogo na ndipo nilipokataa kwa kuwa kipimo ni hicho, lakini walikataa kulipa,” Saidi alisema.

Alidai kuwa baada ya mzozo kuibuka, mteja mmoja aliyekuwa ndani ya duka lililopo karibu na biashara hiyo, aliwasili na kuulizia kuhusu malipo huku akiwa amelewa na kuanzisha vurugu, lakini ghafla gari la Polisi lilifika kwenye eneo hilo na kumbeba hadi kwenye kituo cha Polisi alikofunguliwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Kwa upande wake, muathirika mwingine wa tukio hilo, Dotto Machunda ambaye ni muuza matunda katika eneo hilo, alisema aliona vurugu katika maeneo ya Darajani na baadaye kuona polisi katika kibanda chake ambao walianza kumpiga na kisha kuondoka na kurejea kwenye eneo hilo baada ya muda mfupi.

“Niliambiwa nivue mkanda na kuwekwa ndani kuunganishwa kwenye makosa, lakini mpaka leo hii sijapata matibabu, niliwaomba PF3 nikatibiwe walikataa wakati nipo ndani na nilipotoka walininyima pia. Nilipokwenda hospitali ya mkoa kutibiwa waliniambia kwa kuwa nimepigwa mpaka PF3, mpaka sasa sijapata matibabu,” alisema Machunda.

Mwenyekiti wa Mtaa lilipotokea tukio hilo, Victor Ochieng, alikiri kujua tatizo hilo na kwamba alikwenda kwenye eneo la tukio kupata maelezo ya wananchi wake kisha kufika Kituo cha Polisi kujua kinachoendelea.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huu, Muliro Jumanne, alikiri kupokea taarifa lakini alieleza kuwa alizozipata zilihusu askari wao kuvamiwa na wananchi.

Alisema hata hivyo uchunguzi unaendelea kubaini wahusika wa tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake, kwa sababu hakuna anayeruhusiwa kufanya vurugu hata kama ni polisi.