ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja,
amesema hatua ya Rais John Magufuli kuzuia
kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini,
imelenga kuminya demokrasia na serikali kutaka
kutokosolewa.
Mgeja, ambaye kwa sasa ni mwanachama wa
Chama cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema),
alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo
haikubaliki katika nchi ya kidemokrasia duniani
kwa kuwa uhai wa vyama vya siasa upo katika
mikutano.
Pia amemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,
Jaji Francis Mutungi, kushughulikia migogoro ya
vyama badala ya kusubiri hadi nchi ikielekea katika
mgogoro mkubwa.
Alisema kauli ya Rais Magufuli kwamba shughuli
za kisiasa hadi mwaka 2020, inakiuka katiba kwa
kuwa mikutano na shughuli za vyama vya siasa
vipo kikatiba.
Alieleza kuwa kinachotokea sasa kwa viongozi wa
upinzani ni kupigania demokrasia hali ambayo
inaweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Serikali inakosolewa kupitia mikutano ya vyama
vya siasa na serikali isitupangie cha kuzungumza.
Kutokana na kauli ya rais tunaonya likitokea lolote
katika mikutano ambayo itafanyika nchi nzima,
kupitia operesheni ya Umoja wa Kuondoa Udikteta
Tanzania (Ukuta), Rais atawajibika iwapo nguvu ya
jeshi polisi itatumika,” alisema.