Header Ads Widget

Mwanafunzi UDOM auawa kwa kupigwa na wenzake Wakati Wakitoka Baa

Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Kitivo cha
Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa
kushambuliwa kwa kipigo na watu wanaosadikiwa
kuwa ni wanafunzi wenzake wakati akitoka klabu
ya pombe (Bar).
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika
eneo la chuo hicho ambapo mwanafunzi huyo
alisikika akipiga kelele ndipo walinzi wakafika na
kumkuta akiwa anagalagala njiani.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema
mwanafunzi huyo ambaye ametokea Musoma
mkoani Mara alishambuliwa kwa kupigwa sehemu
mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika.
Amebainisha mwanafunzi huyo alikutwa majira ya
saa 10 alfajiri katika eneo hilo la chuo hicho huku
akisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa
marehemu huyo alikuwa na ugomvi na watu hao
katika klabu ya pombe ya Canival Pub iliyopo
chuoni hapo.
“Alipoondoka kurudi bwenini akiwa njiani
alishambuliwa na watu hao wasiofahamika na
kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake,
kipigo kilichosababisha kifo chake wakati
alipokimbizwa kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Dodoma,” alisema Mambosasa
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa
katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi na hadi
sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na
tukio hilo.
Alipoulizwa kuwa taarifa za mwanafunzi huyo
kushambuliwa na wenzake, Mambosasa alisema
kwasababu inadaiwa haifahamiki upelelezi bado
unaendelea.
“Kwa sababu mwenye bar si yupo, kama kuna
ugomvi ambao ulikuwa unaendelea tutajua tu,
nimemuelekeza OCD kufuatilia ni nani waliokuwa
wanakunywa kwenye hiyo bar chuoni, ni lazima tu
watakuwa wanachuo ili tuwabaini,”
Kamanda huyo amesema ameelekeza uchunguzi
wa kina ufanyike kama kulikuwa na ugomvi ndio
hao hao walienda kumtegea njiani.
Chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutaja jina
lake kwa madai kuwa siyo msemaji wa polisi
kimesema kuwa marehemu Joseph alikuwa
anakunywa pombe pamoja na marafiki zake lakini
baada ya kulewa walianza ugomvi ambao hata
hivyo waliamuliwa.
“Baada ya kuamuliwa ule ugomvi wa awali ndipo
wenzake walipokwenda kumsubiria kwa mbele
kwenye kichaka ambapo walimvamia na
kumshambulia na kumwacha karibu ya kufa,”
kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa, baada ya kumwacha hapo na
kutoweka ndipo walinzi wa chuo hicho waliokuwa
doria walimuokota na kumfikisha kwenye kituo
kidogo cha polisi kilichopo Chimwaga ambapo
alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma alipofariki wakati akipatiwa matibabu.
Chanzo hicho kimesema hakuna mtuhumiwa hata
mmoja anayeshikiliwa na polisi kwa kuwa wote
waliomshambulia walitoroka na hawajulikani
walipo.

Post a Comment

0 Comments