MTUNZI: ENEA FAIDY
..Baada ya kutazama kioo cha simu Mr Alloyce
alishtuka kidogo baada ya kukuta namba ya
shemeji yake. Aliitazama kwa muda, huku
akitafakari jibu la kumpa shemeji yake kwani tayari
alimtaarifu kwamba aje kesho yake asubuhi.
Aliamua kupokea simu ile huku akivuta pumzi
ndefu na kuishusha taratibu sana.
"Halloo Shem! mbona ulikata simu kabla
hujaniambia kuna tatizo gani?" Alisema Bi Sandra
Dada wa mama Eddy.
"Ah..ah..Shem.. Usije kesho... Nimetatua ..tayari
Shem!" Mr Aloyce alijikuta anapata kigugumizi cha
ghafla kwani hakuwa na jibu sahihi la kumjibu
shemeji yake.
"Umetatua SAA ngapi? Mbona sikuelewi shemeji?
Si umesema nije kesho?" Sandra alishangaa.
"Ha..hapana Shem usije kwanza.. Usije!"
"Shem sikuelewi.. Nitakuja kesho.."
Alisikika Sandra kisha simu ikakatika.
Usiku ulikuwa ni mrefu sana kwa familia ile ya Mr
Aloyce, walikesha wakiwa sebuleni yeye na
mwanae. Usingizi ulimpitia kwa dakika chache
kisha akashtuka. Akatazama saa yake ya mkononi
ilikuwa tayari ni Saa kumi na moja alfajiri.
Mr Aloyce aliinuka kitini na kwenda bafuni, alioga
haraka kisha akaingia chumbani na kubadili nguo.
Hakutaka kujichelewesha sana, akarudi sebuleni na
kumuaga Eddy.
"Naondoka Eddy!"
"Baba naogopa kubaki peke yangu!"
"Jitahidi Mwanangu, siwezi kuondoka na wewe!"
"Twende wote baba!"
Eddy alizidi kumkazania baba yake lakini Mr
Aloyce hakukubali hata kidogo kuondoka nae
kwani alihofia misukosuko ambayo ingejitokeza
wakiwa huko.
"Baki na mlinzi basi!"
Eddy aliinuka na kutoka na baba yake, nje
kulikuwa bado hakujapambazuka vizuri hivyo
kulikuwa na kigizagiza ingawa walisaidiwa na
mwanga wa taa.
Mr Aloyce alichukua gari yake nyingine na
kuiwasha haraka kisha akapiga honi ili mlinzi
afungue geti.
"Bosi mbona usiku? Unaenda wapi?" Aliuliza
mlinzi.
"Hayakuhusu.. Fungua geti nitoke, baki na Eddy!"
"Sawa bosi wangu.. Samahani kwa maswali!"
Alisema mlinzi kisha akafungua geti Mr Aloyce
akatoka na kuelekea kule alikopotelea mkewe.
Eddy alibaki na mlinzi wao pale nje, alikuwa na
mawazo mengi sana kichwani hivyo alikuwa
amejiinamia kimya tu bila kuzungumza chochote.
"Eddy mbona unawaza sana?" Aliuliza mlinzi.
Lakini Eddy hakujibu kitu akabaki kimya
amejiinamia.
"Eddy si naongea na wewe husikii au?" Aliuliza
tena kwa sauti ya ukali kidogo. Safari hii Eddy
aliinua kichwa na kumtazama.
"Demu wako amekutosa nini? Maana sielewi elewi
humu ndani.. Mara mtoke mara muingie kimaajabu
ajabu siwaelewi kabisa.!"
"Yanakuhusu?"
"Yanaweza kunihusu kwa sehemu.. !" Alisema
mlinzi yule kwa masikhara.
"Sitaki kelele.." Alisema Eddy na kujiinamia.
"Sikia Eddy... Mnanionaga chizi chizi sana ila nina
akili zangu... Tatizo lako nalijua na ninaweza
kukusaidia.... Sasa endelea hivohivo... Ila jua
mficha uchi hazai..!" Alisema mlinzi kisha
akasogea pembeni na kuchukua shuka lake ili
ajifunike.
"Anko! Umesemaje?"
"Sijasema chochote ..!"
"Anko nisamehe.. Umesema unaweza kunisaidia
tatizo langu?"
"Ndio na ni kazi ndogo... Ila endelea kunifanya
mwehu kila siku....!"
Eddy alimtazama mlinzi wao kwa mshangao wa
hali ya juu.
==>Endelea Nayo <<Kwa Kubofya
Hapa>>