Header Ads Widget

Mzee jela miaka 15 kwa kumiliki silaha Kinyume cha Sheria

Mkazi mmoja wa jijini hapa, Said Shomari (64)
amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya
kupatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha
sheria.
Shomari ambaye ni fundi saa, alitiwa hatiani na
kuhukumiwa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri aliyekuwa
akisikiliza kesi hiyo baada ya mshtakiwa kukiri
kosa hilo.
Alikiri kutenda kosa hilo jana alipopandishwa
kizimbani mahakamani hapo na Wakili wa Serikali
Adolf Mkini kumsomea mashtaka yaliyokuwa
yakimkabili kwa lengo la kumkumbusha, wakati
kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.
Katika kesi hiyo, Shomari alishtakiwa na mtoto
wake, mfanyabiashara Ramadhani Said (40), kwa
makosa mawili, moja la kukutwa na silaha na la
pili la kukutwa na risasi bila kibali na kinyume cha
sheria.
Katika mashtaka hayo, Shomari alikiri kosa moja la
kumiliki silaha na akakana kosa la kumiliki risasi
kinyume cha sheria.
Hata hivyo, wakati Shomari akikiri kutenda kosa
hilo moja na kuhukumiwa adhabu hiyo, mtoto
wake alikana kutenda makosa hayo yote.
Awali, akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Mkini
alidai kuwa Novemba 9, 2015, eneo la Kigogo,
wilayani Ilala, mshtakiwa alikutwa akimiliki bastola
moja ndogo pamoja na risasi moja bila kuwa na
kibali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo na kuulizwa
kama ni kweli au si kweli, ndipo alipokiri kutenda
kosa hilo kwa kujibu kuwa ni kweli, hivyo
Mahakama ikamtia hatiani.
“Kwa kuwa mshtakiwa amekiri kutenda kosa kwa
shtaka linalomkabili, Mahakama inamtia hatiani na
kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela.”,
alisema hakimu Mashauri.
Baada ya kutoa hukumu hiyo aliahirisha kesi hiyo
hadi Agosti 15, mwaka huu, wakati kesi hiyo
itakapoendelea kusikilizwa shtaka moja kwa
upande wa Shomari na mashtaka yote mawili kwa
upande wa Ramadhani.

Post a Comment

0 Comments