Watu 14 wamefariki dunia katika wilaya za
Chemba mkoani Dodoma na Kiteto mkoani
Manyara kutokana na ugonjwa unaojulikana
kitaalamu kama ‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na
sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka
iliyoharibika.
Hayo yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu
ya magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine
leo jijini Dar es Salaam.
“Ugonjwa uliosababishwa na sumu kuvu
(Aflatoxins) uliripotiwa kwa mara ya kwanza tarehe
13 Juni, 2016 katika wilaya za Chemba mkoani
Dodoma na baadaye mkoani Manyara katika wilaya
ya Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza
kuwa:
“Wagonjwa walikuwa na dalili za kuumwa tumbo,
kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na kuwa
manjano sehemu mbalimbali za mwili ambayo
inaashiria kuathirika kwa ini”
Alisema mbali na vifo hivyo, hadi kufikia Julai 31
mwaka huu wagonjwa 54 waliripotiwa kuugua
ugonjwa hu huku wagonjwa wanne wakilazwa
kutokana na kuugua.
“Hadi kufikia tarehe 31, July 2016 kulikuwa na
wagonjwa 54 na watu 14 walipoteza maisha
kutokana na ugonjwa huo.Aidha katika wiki iliyopita
aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya kutoka wilaya ya
Kondoa” alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:
“Jumla ya wagonjwa waliolazwa wodini ni wanne
kati yao mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma
na watatu wapo katika Hospitali ya Kondoa”
Waziri Ummy alitaja wilaya zilizoripoti wagonjwa
hao na idadi ya wagonjwa kuwa ni wilaya ya
Chemba wagonjwa 38, Kondoa wagonjwa tisa ,
Kiteto wagonjwa watatu, Chamwino wagonjwa
wawili na Dodoma Manispaa mgonjwa mmoja.
“Vijiji vilivyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni kutoka
wilaya ya Chemba ambavyo ni Kinkima, Itolwa,
Mwailanje na katika wilaya ya Kondoa ni kijijini cha
Ubembeni” alisema Waziri Ummy.
Hivyo, aliitoa hofu familia iliyopoteza watu wanne
katika kijiji cha Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo
havihusiani na uchawi au kuwekewa sumu bali ni
chakula cha siku ile kilithibitika kwamba kilikuwa
na sumukuvu.
Kufuatia athari hizo Serikali itafanya uchunguzi wa
kina katika wilaya kumi za Chemba, Kondoa,
Chamwino na Kiteto na wilaya nyingine za mikoa
ya Sindida, Dodoma na Manyara zinazopakana na
wilaya hizo.
Alisema uchunguzi huo unalenga kubaini hali ya
usalama wa vyakula vinavyotumiwa na jamii ili
kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kuwaathiri
wananchi wengi zaidi wanaoishi katika wilaya hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Afya
wa Wizara hiyo Dkt. Fausta Mosha alisema wizara
imeandaa vipepereshi vyenye maelekezo
yanayotoa elimu juu ya kijikinga kwa kuandaa
chakula kuanzia hatua ya uvunaji shambani hadi
wakati wa kula.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Otilia
Gowelle alisema njia bora ya kupambana na
ugonjwa huo ni kuukinga kwa kuhakikisha sumu
kuvu haizalishwi kutoka kwenye nafaka.
Akifafanua kuhusu udhibiti, Waziri Ummy alisema
wanashirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na
Uvuvi kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi
ya uhifadhi na uandaaji wa chakula utakaosaidia
kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa nafaka
ambazo hazijaharibika sana.
“Njia hizi ni pamoja na kuhifadhi nafaka zilizokauka
vizuri na kuchambua nafaka zilizoharibika
(zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa
mahindi kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka
zitakazoonekana kuharibika rangi” alisema.
Waziri Ummy alisisitiza Serikali kuendelea
kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza
uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni
pamoja na kujenga uwezo wa kupima sumukuvu
katika damu na choo kidogo miongoni mwa taasisi
za ndani ya nchi.
Inaelezwa kuwa ugojwa
wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na sumu kuvu
(Aflatoxins) kwenye nafaka uliwahi kutokea nchini
Kenya mwaka 2004 na kusababisha vifo vya zaida
ya watu 100 huku wengine 200 waliathirika
0 Comments
on