Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wote
wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji hapa
nchini kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa
na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo
kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi
mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 01
Agosti, 2016 katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na
kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere
Mkoani Geita.
Katika agizo hilo Dkt. Magufuli amewaonya
walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu
kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko
idadi halisi kwa lengo la kupata mgao mkubwa wa
fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua
hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya
hivyo.
"Ninafahamu mgao wa fedha hizo hutolewa
kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo
baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika
wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe
hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo,
wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule
yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela
zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki
moja wagawane.
"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima,
mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo,
msijaribu kula hela ya Serikali" Amesema Rais
Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia ametaka
viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha
wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule
zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha
ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia
sasa ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na
kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu
itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na
wadhifa alionao.
"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa, Mkuu wa
Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu
Tarafa, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila
mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika
shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela
ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki
kutoa hela ambayo haitakiwi" Amesisitiza Rais
Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano
huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na
Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi
yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka
viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza
wajibu wao kwa kutembelea wananchi
wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi
ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika
maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu
unaotumiwa na Halmashauri nyingi za Majiji,
Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika
ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri akisema
mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo
kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi
kidogo katika Halmashauri husika.
"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa
wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni
kwa ajili ya kukusanya fedha? Amehoji Dkt.
Magufuli na kuongeza kuwa;
"Tena mawakala wengine ndio hao hao wamekuwa
wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge
wenye vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila
hata kuwaonea huruma"
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe
Mama Janeth Magufuli amemaliza ziara yake ya
siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora,
Shinyanga na Geita na yupo nyumbani kwake
Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Chato