MWALIMU Daniel Msalika (42) wa shule ya msingi
Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu
amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando alikokuwa amelazwa akitibiwa majeraha.
Majeraha hayo yalitokana na kushambuliwa na
baadhi ya wananchi kwa madai ya kujihusisha
kimapenzi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo
Lyanga aliwaeleza waandishi wa habari jana ofisini
kwake kuwa mwalimu huyo alifariki dunia Julai 31
mwaka huu saa nane usiku.
Kamanda Lyanga alisema kuwa siku ya tukio Julai
27 mwaka huu saa 6.30 usiku, wananchi hao
ambao idadi yao haijafahamika, walivamia nyumba
ya mwalimu huyo baada ya kupata taarifa kuwa
kuna mwanafunzi ambaye amelala nyumbani
kwake, jambo ambalo halikuwa la kweli.
“Wananchi hao walipata taarifa ya kuwa nyumbani
kwa mwalimu kuna mwanafunzi ambaye amelala
humo hivyo walimvamia kwa kuvunja mlango na
kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha
mbalimbali za jadi na kumsababishia majeraha
makubwa sehemu za kichwani na usoni lakini binti
waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18
na siyo mwanafunzi,” alisema.
Alisema kuwa baada ya uvamizi huo, mwalimu
huyo alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Isanga
kupatiwa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa
mbaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando jijini Mwanza, lakini alifariki dunia.
Kamanda alisema kifo chake, kimesababishwa na
majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi
yake zikiwa si za kweli.
Alitoa mwito kwa wananchi kuacha kujichukulia
sheria mikononi huku wakisisitiza kuwa wote
watakaobainika kusababisha kifo hicho, sheria
itachukua mkondo wake.
0 Comments
on