WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto imewataka wananchi na wadau
kutoa taarifa, iwapo kuna mashirika yasiyo ya
kiserikali (NGOs) zinazojihusisha na kuhamasisha
vitendo vya ushoga nchini ili hatua stahiki
zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.
Agizo hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
Msajili wa NGOs, Marcel Katemba. Alisema kuwa
siku za hivi karibuni, kumekuwepo na tuhuma za
kuwepo kwa baadhi NGOs kujihusisha na
kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini.
Alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa NGOs
zinasajiliwa kwa lengo la kutekeleza majukumu
yanayokubalika kisheria na kwamba vitendo vya
kuhamasisha ushoga si majukumu halali
yanayopaswa kutekelezwa.
“Tunazitaka NGOs kutekeleza majukumu yaliyo
ndani ya usajili wao na kuepuka vitendo vya
uvunjifu wa sheria kwani kinyume na hayo hatua
zitachukuliwa,” alisema Katemba na kusisitiza
kuwa vitendo vya ushoga havikubaliki nchini kwani
ni kinyume na mila, desturi na sheria za nchi.
Alisema katika kudhibiti uwepo wa vitendo hivyo,
wadau na umma kwa ujumla wanapaswa kutoa
taarifa zitakazowezesha kuthibitisha tuhuma hizo ili
hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Katemba alisema taifa lina mila, desturi na sheria
za nchi ambazo imekuwa ikizisimamia na
kuzitekeleza na kuhamasishwa kwa vitendo hivyo
kunakwenda kinyume na misingi, ambayo kwa
namna moja vinaweza kuathiri kizazi kwa kizazi.
Alisema ni wakati sasa kwa kila NGO kusimamia
utekelezaji wa majukumu yake kama ilivyosajiliwa,
kuongeza ushiriki wake kwa kutoa michango yao
katika kuleta maendeleo kwa jamii.
Alisema taratibu za usajili wa NGOS chini ya sheria
mashirika yasiyo ya kiserikali namba 24 ya mwaka
2002, yameimarishwa vyema na kila shirika
linalokuwa limepata usajili ni muhimu kutekeleza
yale yaliyokusudiwa ili kuepuka taifa kuingia katika
vitendo visivyostahili.
0 Comments
on