Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi
Wilayani Ilemela kwa tuhuma za kujiunganishia
umeme kinyemela kwenye nyumba zao kinyume na
utaratibu uliowekwa na TANESCO.
Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza
imesema kuwa mnamo tarehe 31.07.2016 majira
ya saa 5:10 asubuhi katika maeneo ya Ilemela
Mlimani wilaya ya Ilemela jiji na mkoa wa
Mwanza, watu watatu wanashikiliwa na jeshi la
polisi kwa tuhuma za kujiunganishia umeme
kinyemela kwenye nyumba zao kinyume na sheria
na utaratibu uliowekwa na TANESCO.
Imewataja watu hao kuwa ni Boniphace Masamaki
miaka 47, Lina Cosmas miaka 26 na Ali Mohamed
miaka 30 wote wakazi wa mtaa wa Ilemela
Mlimani.
Aidha watuhumiwa hao waliweza kukamatwa
baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa raia
wema, ndipo jeshi la polisi kwa kushirikiana na
maofisa wa TANESCO waliweza kufanya msako
maeneo hayo na kufanikiwa kuwakamata
watuhumiwa hao.
Watuhumiwa wote wapo katika mahojiano na jeshi
la polisi wakishirikiana na TANESCO, pindi
uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa
mahakamani.
Msako wa kuwasaka watu wengine ambao
wamejiunganishia umeme kinyume na utaratibu
bado unaendelea.
Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu
Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito
kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza akiwataka
kuacha tabia ya kujiwekea umeme kinyemela
katika nyumba zao kwani ni kosa la jinai lakini pia
wanahatarisha maisha ya familia pamoja na mali
zao.
Amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na
wananchi wema na maofisa wa TANESCO
litahakikisha linawasaka na kuwatia nguvuni watu
wote wanaodaiwa kujiwekea umeme kinyemela
kwenye nyumba zao na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria.