WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amevitaka
viwanda vya sukari nchini kuongeza mikakati ya
uzalishaji zaidi ili mwaka 2020 Tanzania iwe
imefikia kiwango cha kuzalisha asilimia 100 ya
mahitaji yake.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumanne,
Agosti 02, 2016) wakati alipotembelea kiwanda
cha sukari cha Mtibwa kilichoko mkoani Morogoro
ambapo amesisitiza viwanda vya ndani vizalishe
zaidi ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka
nje ya nchi.
Amesema Serikali imejikita katika kuimarisha na
kulinda viwanda vya ndani nchini hivyo ni vema
viwanda vya sukari vikaweka mikakati ya kuzalisha
kwa wingi ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa
hiyo kutoka nje.
“Kiwango cha mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya
tani 400,000, nimeiagiza Bodi ya Sukari kukaa na
wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
na kufanya utafiti ili tujue mahitaji halisi ya sukari,”
alisema.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mkakati
wa kulinda viwanda vya ndani kwa kuziongezea
kodi bidhaa zinazotoka nje ambazo zinazalishwa
na viwanda vya ndani ikiwemo sukari hivyo wenye
viwanda hawana budi kuzalisha kwa wingi zaidi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa
viwanda vya sukari nchini kutoa motisha kwa
wakulima wa nje kwa kununua miwa yao kwa bei
nzuri na kuwalipa kwa wakati ili nao wanufaike na
uwepo wa viwanda hivyo na kuwa walinzi wa
uwekezaji huo.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano Mwandamizi
wa kiwanda hicho, Ibrahim Juma amesema kwa
sasa kiwanda kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka
na wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani
70,000 ifikapo mwaka 2021.
Juma alisema uzalishaji wa sukari kiwandani hapo
ulipungua kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka
nje hivyo aliipongeza serikali kwa kudhibiti
uingizwaji holela wa sukari kutoka nje jambo
litakalosaidia ukuzaji wa viwanda vya ndani.
Meneja huyo alisema kuwa kwa sasa wameanza
upanuzi wa mashamba kiwandani hapo ambapo
wanatarajia kuongeza hekta 400,000 lengo likiwa
ni kutimiza ndoto ya Serikali ya kuifanya Tanzania
ijitosheleze katika uzalishaji wa sukari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 Comments
on