Header Ads Widget

Dereva Ajali ya City Boy Iliyoua watu 30 Ajisalimisha Polisi

MMOJA wa madereva waliosababisha ajali ya
mabasi ya Kampuni ya City Boy iliyotokea Julai 4,
mwaka huu na kutoroka, Boniface Mwakalukwa
(37), amejisalimisha mikononi mwa polisi na
kufikishwa mahakamani.
Mwakalukwa ambaye ni mkazi wa jijini Dar es
Salaam jana aliunganishwa kwenye mashitaka na
dereva mwenzake Jeremiah Semfungwe (34) wote
kwa pamoja wakikabiliwa na makosa 30 ya kuua
bila kukusudia.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida,
Joyce Minde ilidaiwa kuwa washitakiwa hao
walitenda makosa hayo Julai 4, mwaka huu saa
8.15 mchana wakati wakiendesha mabasi aina ya
Scania yenye namba za usajili T 247 BCD na T 331
DCE kwa kuyagonganisha.
Ilidaiwa kuwa kitendo hicho ambacho kilitokea
Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni kilisababisha
vifo vya abiria 30 na majeruhi 54. Wakili wa
Serikali, Petrida Muta alidai kuwa siku ya tukio
watuhumiwa wakiwa ni madereva wa Kampuni ya
City Boys, bila kukusudia, walisababisha vifo vya
abiria hao kinyume na Kifungu 195 na 198 cha
Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.
Ingawa Wakili wa washitakiwa, Francis Kitope
aliiomba Mahakama iwape wateja wake dhamana
kwa kuwa chini ya Kifungu 148 cha Mwenendo wa
Makosa ya Jinai, kosa hilo linadhaminika, Wakili
wa Serikali Muta alipinga dhamana hiyo.
Muta ambaye aliwasilisha Hati ya Kiapo mbele ya
Mahakama hiyo, alidai kuwa kwa kufanya hivyo
usalama wa washitakiwa utakuwa hatarini kwa
kuwa ndugu wa marehemu na majeruhi bado wana
hasira kutokana na ajali hiyo kuwa bado
haijasahaulika.
Aidha, Muta aliendelea kudai kuwa baadhi ya
majeruhi wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na
hatma yao haijulikani, hivyo si vyema washitakiwa
kupewa dhamana wakati huu. Kutokana na
upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika, washitakiwa
wamerejeshwa rumande hadi Agosti 4, mwaka huu
kesi yao itakapotajwa tena

Post a Comment

0 Comments