WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku moja
kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro kutenga
maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara
wadogo na kuyatangaza kesho ( leo ).
“Mbali na kutenga maeneo pia nawaagiza
muwasaidie wafanyabiashara hawa kuunda vikundi
kulingana na aina ya biashara wanazozifanya ili
kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi kutoka
katika taasisi za fedha” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumatano,
Agosti 03, 2016) wakati alipotembelea mradi wa
ujenzi wa kituo cha mabasi Msamvu unaojengwa
kwa ubia kati ya Manispaa ya Morogoro na Mfuko
wa Pensheni wa LAPF.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa
kufunguliwa Agosti 12 mwaka huu utakuwa ni
kituo cha mabasi cha kwanza cha kisasa Tanzania
ambapo Waziri Mkuu amezitaka halmashauri zote
zilizoko makao makuu ya mikoa nchini kuiga
mfano huo.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kulipongeza
Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro na
LAPF kwa kubuni mradi huo wa kisasa utawezesha
abiria kupata taarifa ya basi lilipo na muda
litakapowasili kituoni hapo hivyo kupunguza
udanganyifu kutoka kwa mawakala wasiokuwa
waaminifu.
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo Stanley
Mhapa alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni
40 ambapo Manispaa inamiliki asilimia 40 ya hisa
na mfuko wa LAPF unamiliki asilimia 60.
“Mafanikio ya mradi huu ni pamoja na kuiwezesha
Manispaa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka
sh 350,000 kwa siku hadi kufikia sh. milioni 1.7
kwa siku,” alisema.
Mhapa alisema mradi huo utakapokamilika utatoa
huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za
kibenki, vibanda vya biashara, sehemu za chakula,
ofisi na sehemu ya mapumziko ya abiria na
vibanda vya kukatia tiketi.
0 Comments
on