MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es
Salaam imewaachia huru wabunge watatu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa
wanakabiliwa na mashitaka ya kuomba rushwa ya
Sh milioni 30.
Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage
aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati
ya kuwafutia mashitaka.
Wabunge hao na majimbo yao katika mabano ni
Kangi Lugola wa Mwibara mkoani Mara maarufu
kama ‘Nyoka wa Shaba,’ Suleiman Saddiq
‘Murad’ (Mvomero – Morogoro) na Victor
Mwambalaswa (Lupa – Songwe).
Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa
Kishenyi akisaidiwa na Wakili Emmanuel Jacob
kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), waliieleza mahakama kuwa
kesi hiyo imetajwa kwa ajili ya washitakiwa
kusomewa maelezo ya awali.
Kishenyi alidai mbali na kutaka kuwasomea
maelezo ya awali washitakiwa hao, DPP anaomba
kuwafutia mashitaka yao kwa kuwa hana nia ya
kuendelea na mashitaka dhidi yao.
Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Mpale
Mpoki aliiomba mahakama itoe agizo ili apewe
maelezo ya mlalamikaji. Hakimu Mwijage alisema,
mahakama imekubali ombi la DPP hivyo kuanzia
sasa wabunge hao wapo huru.
Aidha, alisema wakili Mpoki anatakiwa afanye
juhudi kwenda katika ofisi za DPP ili kupata taarifa
hizo, kinyume cha hapo mahakama haiwezi kutoa
amri kwamba apatiwe maelezo hayo.
Baada ya washitakiwa hao kuachiwa huru, ndugu
na marafiki wa wabunge hao waliokuwa wamefika
mahakamani, walianza kuangua kilio cha furaha.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake,
Lugola alisema watakaa na wanasheria hao ili
wajue nini cha kufanya kutokana na udhalilishaji
waliofanyiwa na Takukuru.
"Tumesikitishwa sana na kitendo cha Takukuru
walivyotufikisha mahakamani na kutushitaki kwa
kashfa ya rushwa na dunia nzima imetambua, lakini
tangu tufike mahakamani mioyo yetu ilimtanguliza
Mungu na leo (jana) Mungu ametoa majibu,”
alisema Lugola.
Alisema walikuwa wanajua kuwa kesi hiyo ni ya
kutunga na ilijaa siasa kwa kuwa awali Takukuru
ilisema upelelezi umekamilika, lakini hawakuwa na
ushahidi na ndio maana wameamua kuifuta.
Kwa mara ya kwanza wabunge hao walipandishwa
kizimbani, Aprili mosi mwaka huu wakidaiwa kuwa
Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne
usiku, katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni
jijini Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa kama
wabunge na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh
milioni 30.
Inadaiwa waliomba fedha hizo kutoka kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa
ya Gairo, Mbwana Magotta, kama kishawishi cha
kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri
hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kupandishwa kizimbani kwa wabunge hao
kulitokana na kashfa ya rushwa iliyomsababisha
Spika wa Bunge, Job Ndugai kupangua wenyeviti
na makamu wenyeviti kwa kuwaondoa kwenye
kamati walizokuwa wanaziongoza. Mabadiliko
hayo yaliwagusa pia wabunge 27, ambao baadhi
yao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
0 Comments
on