Siku tatu baada ya kutuliza vurugu baina ya viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM), polisi inamshikilia mwenyekiti wa umoja huo, Lengai Ole Sabaya kwa tuhuma za kughushi kitambulisho cha Idara ya Usalama wa Taifa.
Viongozi hao walipambana Alhamisi wiki hii wakati wakigombea ofisi ya umoja huo ya mkoa, vurugu zinazodaiwa kusababishwa na mgogoro wa chini kwa chini uliodumu kwa miezi miwili kati ya makundi mawili yanayokinzana.
Wakati hali hiyo haijatulia, juzi saa 6.00 usiku, Sabaya alikamatwa katika baa ya Mile Stone akiwa na wenzake.
Habari zilizopatikana jijini Arusha zinasema kitambulisho hicho kilipelekwa kituo kikuu cha polisi ambako kulifunguliwa jadala la kesi ya madai namba RB 5055/2016. Ilifunguliwa na hoteli ya Sky Way aliyokwenda kulala na kuondoka bila kulipa gharama za malazi.
Awali, ilidaiwa kwamba mwenyekiti huyo aliweka rehani kitambulisho hicho na simu yake ili kupewa muda wa kulipa deni la hoteli hiyo.
Meneja wa hoteli hiyo, Filipo John alisema kiongozi huyo alikuwa akidaiwa Sh309,400 za siku sita alizolala hotelini hapo.
Pia, John alikiri kupokea kitambulisho hicho na simu ambavyo alisema baada ya kiongozi huyo kuondoka bila kulipa, alipeleka malalamiko kwa uongozi wa mtaa na baadaye alipeleka kesi hiyo polisi.
“Nilipeleka kesi kwa balozi na mwenyekiti wa mtaa, lakini walishauri vitu vyake vipelekwe polisi. Baada ya kunilipa nilifuta kesi,” alisema meneja huyo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo alisema wanaendelea kumshikilia Ole Sabaya kwa ajili ya upelelezi na atafikishwa mahakamani kesho.