Mamlaka ya  Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezuia uingizwaji na usambazaji nchini wa simu aina ya Samsung Galaxy Note 7 kutokana na matatizo ya simu hizo kulipuka.

Agizo hilo limetolewa na Meneja Mawasiliano wa TCRA akiwataka watumiaji wa simu hizo kuzirudisha walikonunua huku akipiga marufuku uingizwaji na usambazaji wa aina hiyo ya simu kwani ni hatari kutokana na matukio mbalimbali ya simu hizo kulipuka yameripotiwa.

Mapema wiki hii Kampuni ya Samsung ya nchini Korea Kusini ilitangaza kuwa haitengeneza tena simu aina ya Galaxy Note 7 kutokana na kuwa na tatizo la betri. Awali tatizo hili liliripotiwa na kampuni hiyo iliagiza simu zote zilizouzwa zirejeshwe kiwandani ili zifanyiwe marekebisho na kuwa wateja hao watapatiwa simu nyingine.

Lakini hata simu zilizotoka awamu ya pili baada ya matengenezo, zilikuwa na tatizo lile lile la kulipuka.

Kampuni hiyo ilitarajia kuwa aina hiyo mpya ya simu iliyozinduliwa ingeisaidia kuweka ushindani na kampuni ya Apple iliyozindua simu aina ya iPhone 7 mwezi uliopita.

Mbali na Tanzania, nchi nyingine pia zimezuia matumizi ya simu hizi na kuwataka wasafiri hasa wanaotumia usafiri wa anga kuhakikisha simu hizo wanazitoa betri, hawazichomeki katika umeme wala kuziwasha wakiwa katika viwanja vya ndege wakati wa safari.
==