Mhasibu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Hamida Masoli  amefikishwa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu  na kupandishwa kizimbani  akikabiliwa na mashtaka 95, yakiwamo ya uhujumu uchumi, ubadhirifu, wizi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh71.7 milioni.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Denis Lekayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage amedai mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la ubadhirifu na ufujaji, shtaka moja la kusababisha hasara, mashtaka 44 ya kutumia ofisi vibaya na kumdanganya mwajiri wake na mashtaka 49 ya wizi.

Lekayo amesema  kati ya Julai Mosi, 2007 na  Desemba 31, 2011 kwenye ofisi za Makao Makuu ya TTCL yaliyopo wilayani  Ilala,  Masoli akiwa mwajiriwa alifuja Sh70,469,407 kwa matumizi yake binafsi. Alidai kati ya Mei 2007 na Novemba 30, 2011 kwenye ofisi za TTCL kwa makusudi mshtakiwa alisababisha hasara kwa Serikali ya Sh71,769,407.

Masoli anadaiwa kati ya Septemba 24 na 30, 2007,  kwa nafasi yake ya mhasibu wa mishahara TTCL, alitumia nyaraka ya uongo kumdanganya mwajiri wake akijaribu kuonyesha Sh567,261,684 zilitumika kwa mishahara ya kampuni  hiyo wakati akijua ni uongo.

Mshtakiwa anadaiwa kwa nafasi yake  kati ya Mei 15 na 30, 2007 aliibia kampuni ya TTCL fedha hizo  ambazo alikabidhiwa kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kumsomea mashtaka, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi unaendelea na kwa kuwa mashtaka yameunganishwa na uhujumu uchumi na kwa mujibu wa hati iliyowasilishwa mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayo mamlaka ya kusikiliza maombi ya dhamana.

Hakimu Mwijage alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao kila mmoja atasaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh20 milioni pia, awe na barua kutoka kwa mwajiri wake. Mshtakiwa ametakiwa kuwasilisha hati yake ya kusafiria Takukuru ndani ya siku saba na katika muda huo asipofanya hivyo atafutiwa dhamana.

Mshtakiwa alikamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa huru. Kesi imeahirishwa hadi  Novemba 8, 2016 kwa ajili ya kutajwa.
==