Jeshi la polisi mkoa wa Singida, linamshikilia askari mgambo mwajiriwa hospitali ya mkoa, MG 7822 Emmanuel Daghau (42) kwa tuhuma ya kutoa taarifa za uongo juu ya maiti kufufuka ikiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa.

Imedaiwa kuwa uongo huo ulizua mtafaruku mkubwa kwa ndugu na jamaa wa merehemu Rahel Erasto (28), aliyekuwa mkazi wa Minga manispaa ya Singida.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Singida, SSP Mayala Towo, alisema tukio hilo limetokea Septemba, 30 mwaka huu, majira ya alasiri huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.

Akifafanua, kaimu kamanda huyo alisema kuwa Septemba, 29 mwaka huu Rahel (marehemu) alifikishwa katika hospitali hiyo ya mkoa, kwa ajili ya kupata huduma za kujifungua salama.

“Kutokana na sababu za kitabibu Rahel, alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo ililazimika kufanyiwa upasuaji ambapo mtoto wa kiume alitolewa akiwa hai, Lakini mama kwa bahati mbaya alifariki dunia usiku saa saba Septemba, 30. Mimba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa marehemu Rahel,” alisema kaimu kamanda huyo.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa baada ya Rahel kufariki dunia, mwili wake ulipelekwa mochwari ambapo kesho yake, ndugu walijikusanya eneo hilo wakijadiliana namna kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuzika.

Alisema kuwa wakati ndugu wakiendelea kuzungumzia masuala ya mazishi, alijitokeza mlinzi Daghau na kuwaeleza kuwa ndugu yao huyo, alifariki kutokana na uzembe na kwamba usiku akiwa kwenye doria za kawaida, alisikia marehemu akipiga chafya na aliposogelea dirishani, alimwona akiwa amefufuka.

Towo alisema kuwa awali mgambo huyo baada ya kuhojiwa na Polisi, alikiri kumwona marehemu huyo akiwa amefufuka na alisikia akipiga chafya. Alikiri kwa maandishi na kuweka saini yake.

Alisema lakini baada ya Emmanuel kubaini kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu na watoa huduma za afya hospitali ya mkoa kudai kuwa Rahel amefariki dunia kutokana na matatizo ya kawaida ya uzazi na wala hakufa na kufufuka, alipohojiwa mara ya pili, alikana maelezo yake ya awali aliyotoa kwa Polisi.

Wifi wa marehemu Rahel, Mary Mpaki, alikiri kuwa alimsikia mlinzi Emmanuel wakati akiwatangazia waombolezaji kuwa marehemu amefariki dunia kutoka na uzembe wa madaktari, na kwamba alipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti akiwa hai.

“Kama ndugu wa marehemu ambao baada ya kufanyiwa upasuaji kuna ndugu ambao walitaka kulala wodini lakini hawakuruhusiwa.Tuliposikia maneno ya mlinzi huyo, tuliamini kwa asilimia mia moja maneno yake kwamba Rahel alipelekwa mochwari akiwa bado yu hai,” alisema kwa masikitiko.

Mary alisema baada ya taarifa ya mlinzi huyo, walienda moja kwa moja kituo cha Polisi kutoa taarifa hizo za kusikitisha.

Ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema taarifa iliyotolewa na mlinzi kuwa Rahel alifufuka na kupiga chafya, zitakuwa ni za ukweli kwa sababu Ni mtu mwenye akili, hawezi kudanganya jambo hilo.

“Tunasikia kwamba mlinzi kala matapishi yake kwa kitendo cha kukanusha taarifa alizotoa awali kituo cha Polisi. Kama amefanya hivyo, itakuwa kuna shinikizo amepata hivyo anatafuta njia ya kujiokoa,” alisema.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa, Dk.Ramadhani Kabala, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kudai kwa sasa mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi, ili kutambua kama kweli Rahel alifufuka na kupiga chafya akiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti.

“Ingawa si rahisi binadamu kufufuka baada ya kufariki dunia, lakini hatuwezi kuzipuuza taarifa hizi za mlinzi. Ipo timu inaongozwa na daktari bingwa kutoka wiraza ya mambo ya ndani, Dk.Ahmed Makata inaendelea na uchunguzi wa kina. Kwa hiyo baada ya kumalizika kwa uchunguzi, tutawaita waandishi wa habari kuwaeleza ukweli ili muweze kuitaarifu jamii,” alisema Dk.Kabala.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, alikiri kupokea taarifa hiyo ya aina yake, na kwamba zipo timu mbili zinaendelea na kuchunguzi ili ukweli uweze kubainika.