Kirusi hichi kinasemekana kuharibu simu janja zenye kutumia programu endeshaji maarufu ya Android na iOS(kwa mara ya kwanza), kimeharibu zaidi ya simu janja milioni 10 na zaidi.

Kwa muujibu wa taarifa kutoka Check Point zinasema kuwa kirusi hicho kina uwezo wa kuathiri simu janja au tablet na kuweza kudukua taarifa mbalimbali muhimu kutoka kwenye barua pepe, taarifa zako za benki na kingine chochote kitakachohitajika ili kuweza kukamilisha uhalifu na kisha kuuza taarifa hizo kwa wezi wa mitandaoni.


Jinsi kirusi hicho kinavyoathiri simu janja/tablet zenye kutumia Android/iOS

Iwapo mtu atatembelea tovuti ambayo siyo ya kweli, kirusi hicho kitajaribu kuingia kwenye simu janja/tablet na kujaribu kupata ruhusa ya kufanya/kuona kila kitu (root access) na ikishindikana kirusi hicho kitajaribu kumuwezeshesha mtu kuweza kufanya karibu kila kitu kwenye tovuti aliyoitembelea mfano unapoambiwa ubonyeze linki fulani kuweza kuangalia video ya ngono.


Kama hayo yote mawili yakishindikana kirusi hicho kitatuma taarifa ya uwongo kukujulisha(notification) uweze ku-update simu janja/tablet yako na ukidanganyika na kuruhusu maboresho kufanyika(updating) basi kirusi hicho kitakuwa kimepata ruhusa ya kudukua taarifa zako na kuziuza kwa wezi.


Taarifa zinasema kuwa Uchina kirusi hicho kimeathiri sana vifaa ya kielekroniki(simu janja/tablet) kwa wingi zaidi, takribani vifaa 1.6m ikifuatiwa na India(1.35m), Marekani ikiwa nafasi ya tatu katika idadi ya simu janja/tablets  ikifuatiwa na Australia na Uingereza kwa pamoja jumla ya vifaa 100,000 vikiharibiwa na kirusi hicho.
 
Chati ikionyesha nchi zilizoathiriwa na kirusi hicho chenye kuathiri simu janja/tablet


Google wanasema kuwa wanataarifa kuhusu kirusi hicho na wamekuwa wakizuia apps zilizokwishaharibiwa na kirusi hicho kuweza kupakuliwa na kuboresha kompyuta zao ili kuweza kuufanya taarifa za wateja wao kuwa salama zaidi.

Iwapo kifaa chako kimeathiriwa na kirusi hiki jambo la kufanya ni kufuta kila kitu(restore factory) kwenye simu janja/tablet. Epuka kupakua app kutoka kwenye tovuti isiyoaminika(kama sio kutoka kwenye app store/apple store).