Magari yanayojiendesha yamezidi kupata kasi katika sekta ya magari, teknolokjia hii pamoja na magari ya umeme ndiyo itatawala sekta ya magari pengine baada ya miaka 10.

Watengenezaji wa magari wengi tayari wamekwisha anza kutengeneza na kuyafanyia majaribio magari yanayojiendesha yenyewe katika nchi mbali mbali na leo kampuni ya VOLVO imetangaza kwamba itaanza kuyajaribu magari yake yanayojiendesha yenyewe nchini Uingereza mwakani.

VOLVO inategemea kuanza na magari kadhaa ambayo yatabeba familia halisi na huku yakiwa na wahandisi nyuma ya usukuani na magari haya yatakuwa yakitumia barabara za umma za nchini Uingereza. Idadi ya magari yatakuwa yanaongezwa taratibu hadi kufikia walau magari 100 barabarani ifikapo mwaka 2018.


Teknolojia ya magari yanayojiendesha na pia yale ambayo yanatumia umeme ni maeneo ambayo ndani ya miaka 10 ijayo yanategemewa kuwa na uendelezwaji mkubwa zaidi kushinda maaeneo mengine. Mawazo ya kuwa na magari ambayo yanajiendesha yenyewe hayajaanza kuja jana ama juzi, historia inaonesha kwamba majaribio ya magari ambayo yanajiendesha yenyewe yalianza tangu mwaka 1920 ambapo ilichukua karibu miaka 60 kupata gari kamili ambalo linajiendesha lenyewe.

VOLVO sio kampuni ya kwanza kufikia hatua ya majaribio ya aina hii ya magari kwani tayari Google na baadhi ya makampuni yamekwishaanza kufanya majaribio ya magari ambayo yanajiendesha yenyewe.



Inaaminika kwamba magari yanayojiendesha yenyewe yatasaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva ambao unatokana na madeleva kuchoka, ingawa pia hili litaja kuwa na madhara kwa kuzidi kupunguza nafasi za ajira.

VOLVO watatumia majaribio haya kuchukua data ambazo zitawasaidia kuboresha magari yanayojiendesha ambayo inayetengeneza, na bado haijajulikana ni njia gani wataitumia kuchagua familia ambazo zitayajaribu magari haya. Bado kampuni hii haijapata majibu ya maombi yake ya kibali juu ya barabara zipi itumie kwa magari haya ila ni wazi kwamba watatumia barabara za A ndani ama kuzunguka London.

Pamoja na London kampuni hii pia itaweka magari katika nchi nyingine kama vile Sweden pamoja na China ili waweze kupata data za miji ambayo inamisululu mikubwa ya magari ambazo zitasaidia kutengeneza gari bora zaidi.