Wakati
Tanzania leo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu kufariki kwa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili,
Ali Hassan Mwinyi amesema Taifa limepoteza mwelekeo kwani halina tena
uadilifu aliotujengea Mwalimu Nyerere.
Mwinyi
aliyerithi mikoba ya urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985,
alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mdahalo wa
kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzindua kitabu cha 'Selective works of
Mwalimu Nyerere', kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China.
Mdahalo
huo uliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na Ubalozi wa China
na Asasi ya Urafiki kati ya Tanzania na China. Mwalimu Nyerere
aliyeitawala Tanzania kwa takribani miaka 24, alifariki dunia Oktoba 14,
1999 kwenye Hospitali ya St Thomas jijini London nchini Uingereza
ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya saratani ya damu.
Aliiongoza
Tanzania kwa uadilifu mkubwa akisimamia misingi ya haki, umoja,
mshikamano, kupiga vita rushwa, kusisitiza kujitegemea na uzalendo kwa
nchi.
“Kazi
za kawaida kweli zinafanywa na zinaendelea, lakini sina uhakika hata
kidogo kama uadilifu aliotuachia Mwalimu bado tunao, sijui nani wa
kulaumiwa,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa. Alisema kwa
namna ambavyo mambo yanakwenda, ni kiashiria tosha kuwa nchi haina
uadilifu tena.
“Mambo yanavyokwenda kama gari lililo katika usukani,”
alieleza Mwinyi na kuongeza kuwa kuna kila sababu ya kutafakari hali
ilivyo sasa ikilinganishwa na ile ambayo iliachwa na Baba wa Taifa miaka
hiyo 17 toka kufa kwake.
Alisema
nafasi hiyo ya mazungumzo katika mdahalo, inawapasa kukaa kutafakari
namna ya kurudisha nchi kwenye reli ambayo iliachwa na Mwalimu Nyerere
ambaye ndiye muasisi wa taifa hili katika misingi ya uongozi.
“Tuna
utajiri wa machoni, lakini ndiyo aliyokusudia Mwalimu? Alitufundisha
tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa moyo? Tujali vitu au tujali utu?" Alihoji Rais huyo mstaafu.
Aidha,
Mwinyi alisema Mwalimu Nyerere aliijenga nchi kwa misingi ya utu na
kwamba alijitahidi sana kusaidia nchi nyingine za Afrika na hasa zile za
Kusini mwa Afrika kujikomboa ili Afrika yote iwe huru.
Alisema
ukombozi huo usiwe wa kuingia msituni kupigana na kuwatisha akinamama
na pia usiwe wa kuwaacha watoto kujilea wenyewe bila kujengewa misingi
ya uadilifu.
“Siku
hizi kuna panya road, wametoka wapi watoto hawa? Sisi wazee hatukuwepo?
Au sisi wazee tumetengeneza mazingira kuwepo hao, mbona mwanzo
hawakuwepo sasa wametoka wapi?" Alihoji tena Mwinyi.
Mwinyi
alihoji pia kama mafunzo ya askari yamebadilika, iweje huko awali
askari alikuwa ni mtu ambaye wananchi walikuwa wakimuona wanamkimbilia
tofauti na sasa ambako wananchi wanamkimbia askari.
Aliongeza
kuwa pia ni wakati sasa wa kutafakari kwa nini nchi pamoja na watu wake
wamefikia walipo sasa kwani kuna tatizo pia la ubaguzi wa kikabila
katika upatikanaji wa ajira mbalimbali pamoja na ubaguzi wa kidini.
Aidha,
alisema kama yatabainika kuwepo mambo hayo, yasiachwe hivyo badala yake
upatikane ufumbuzi ili kurudisha yale yote mema ambayo yaliachwa na
Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kuikomboa nchi, uongozi wake na
pia usia wake.
"Baba
wa Taifa kwangu alikuwa zaidi ya kiongozi, alikuwa kaka, rafiki na mtu
aliyegeuza maisha yangu na kunifanya kuwa hivi nilivyo sasa, nimejifunza
mambo mengi na nisipoyafuata itakuwa hasara kwangu,” alisema Mwinyi mmoja wa viongozi wastaafu wanaoheshimika na kupendwa na Watanzania.
Kwa
upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph
Semboja alisema taasisi hiyo inaamini mdahalo huo utazaa maarifa na
kuleta majibu ya changamoto ya karne ya 21.
“Mwalimu leo hii hayupo lakini mawazo na falsafa zake vinaishi na sisi hivyo ni vyema tuvitumie katika vizazi vijavyo,” alisema Profesa Semboja.
Mtendaji
Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema Mwalimu
Nyerere alitujengea misingi ya kujenga taifa katika msingi wa watu na
tabia zao na sio vitu kama vile majengo, madaraja na mengineyo.
Alisema
mdahalo ule haukuwa kwa ajili ya kutazama kifo cha Mwalimu Nyerere,
bali kutazama mambo ya msingi ya kulisaidia taifa kusonga mbele.
Katibu
Mkuu wa Asasi ya Urafiki China na Tanzania, Joseph Kahama alisema nchi
mbalimbali za Afrika zimekuwa zikibadili katiba za nchi zao na viongozi
kujiongezea muda wa utawala, lakini nchini mchakato wa Katiba umedorora
kabisa.
0 Comments
on