Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amempongeza Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro kwa kuteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja huo Sudan Kusini.

Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro ameteuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali ambaye amemaliza muda wake.

Katika pongezi hizo Rais Magufuli amesema Tanzania imepokea uteuzi huo kwa heshima kubwa na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitaji kwa Balozi Joram Mukama Biswaro katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Natambua kazi kubwa iliyopo mbele yako katika nafasi hiyo muhimu ndani ya Umoja wa Afrika (AU), hata hivyo kwa kutambua uwezo wako, uzoefu wako na uchapakazi wako naamini kuwa utatekeleza majukumu yako kwa viwango vya hali ya juu na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma hatajutia uamuzi wake wa kukuteua katika nafasi hiyo”amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amemtakia heri Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro katika majukumu hayo mapya, na amemshukuru na kumpongeza Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali aliyemaliza muda wake kwa uwakilishi mzuri katika kipindi chake.

Aidha, Rais Magufuli ambaye ndiye aliyempendekeza Balozi Prof. Joram Mukama Biswaro kushika nafasi hiyo, amemshukuru Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma kwa kuridhia mapendekezo yake.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

04 Oktoba, 2016