Sakata la posho za madiwani wa Jiji la Arusha bado halijapoa, baada ya Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kuliibulia katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), akisema linakwamisha ukusanyaji wa mapato. 
Sakata hilo liliibuka jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipitia na kuhoji hesabu za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015. 
Mbunge huyo alisema halmashauri hiyo imekata posho kwa madiwani na watendaji na kuzipeleka fedha hizo kwa walimu, jambo ambalo linawavunja moyo wawakilishi hao wa wananchi kutimiza majukumu yao. 
“Madiwani ndiyo wanawasaidia kuwahamasisha wananchi katika ukusanyaji wa mapato na hao mnawavunja moyo. Mkurugenzi hamuwezi kufikia malengo kama mtakuwa watendaji peke yenu,” alisema Selasini. 
Alisema halmashauri hiyo ikimaliza mvutano huo inaweza kuongeza mapato kutoka Sh12 bilioni hadi Sh18 bilioni na kujiendesha bila kutegemea ruzuku. 
Mbunge huyo alisema katika halmashauri zote nchini hakuna diwani anayelipwa posho ya Sh10,000, kwa nini madiwani wa jiji hilo pekee walipwe kiasi hicho. 
Akijibu hoja hiyo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Athuman Kihamia alisema hakuna diwani anayelipwa kiasi hicho cha fedha na kwamba, madiwani wote wanalipwa posho ya Sh40,000 kwa mwezi na nauli Sh10,000 kulingana na kanuni walizokubaliana mwaka 2003. 
Alisema madiwani hao walikuwa na posho zipatazo tano ambazo ni nauli, kujikimu, vikao, madaraka na mawasiliano.

Pia, Kihamia alisema walikuwa wakilipwa Sh150,000 za mafuta kinyume na kanuni walizokubali kuzitumia za mwaka huo. 
“Siwezi kurudia makosa kwa kulipa fedha zisizofuata kanuni na utaratibu, maana mtakuja kunihoji hapa kwa nini nimezilipa,” alisema. 
Mbunge wa Kwela (CCM), Ignas Malocha alimpongeza mkurugenzi huyo kwa kufuata misingi na utaratibu wa kanuni na sheria katika uendeshaji wa jiji hilo.
 Akizungumza nje ya kamati hiyo, Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro alitaka liachwe lijiendeshe lenyewe bila kuingiliwa.

==