Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imemkuta na hatia mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee kumkashifu Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga pamoja na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba.

Hukumu hiyo imesomwa mahakamani hapo kufuatia kesi iliyokuwa imefunguliwa na viongozi hao wawili wa Clouds Media Group wakimtuhumi Judith Wambura kuwakashifu na kuwaharibia taswira zao na kampuni yao katika jamii.

Awali mahakama hiyo ilipanga kusoma hukumu ya kesi hiyo ya madai Oktoba 13 mwaka huu lakini Hakimu Lyamwike aliiahirisha hadi Novemba 2 mwaka huu kwa maelezo kuwa hakuwa amemaliza kuiandikia hukumu.

Katika kesi ya msingi, Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba waliiomba mahakama itamke kuwa maneno yaliyotolewa na Judith Wambura kubitia blog yake ni kashfa na yanaathiri taswira yao katika jamii, pia mahakama imuamuru aombe radhi kupitia vyombo vya habari na alipe fidia kutokana na madhara ya jumla kwa jinsi mahakama itakavyoona inafaa.

Judith Wambura aliandika waraka katika blog yake na kwenye baadhi ya magazeti uliokuwa na kichwa cha habari “Wosia wangu ikitokea nimetangulia kufa kabla ya Ruge na Kusaga.”

Wakati akijibu shtaka hilo, Wambura ambaye alikuwa mtetezi pekee wa upande wake alikiri kuandika waraka huo, hivyo mahakama imemtaka aombe radhi kwenye chombo cha habari chenye coverage kubwa hapa  nchini na ikiwezekana duniani pia
==