Header Ads Widget

Muhimbili yafanya upasuaji Mkubwa wa kihistoria wa Kuhamisha Misuli

Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili jana kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji kwa kutumia darubini (microvascular surgery) wa kuhamisha misuli na mishipa ya damu kutoka kwenye mguu kwenda sehemu nyingine chini ya mguu (free gracilis muscle transfer).

Upasuaji huu wa aina yake na ambao mara nyingi huchukua muda wa saa sita hadi saba una lengo la kujenga uwezo kwa watalaamu wa ndani ili waendelee kutoa huduma za ubingwa wa hali ya juu kwa Watanzania wengi zaidi na vilevile kupunguza kasi ya kupeleka wagonjwa nje.

Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye pia ameshiriki upasuaji huo Dk Ibrahim Mkoma alisema upasuaji huo unagharimu kiasi cha dola 40,000 za Marekani nchini Australia ikiwa ni gharama ya upasuaji tu.

Lengo kubwa la ushirikiano wa upasuaji huu ni wataalamu kutoka Australia kuwaachia taaluma ya upasuaji huo madaktari MNH ili iweze kuendelea kufanya upasuaji huo mbeleni.

Aidha Dk Mkoma alisema kuwa kuanzia mwakani kutakuwa na utaratibu ambao utaanzishwa Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, wa taaluma maalumu ya kusomea upasuaji wa aina hiyo ili kuweza kupata wataalamu zaidi kutoka nchini. Alisema hakuna chuo chochote Tanzania kinachotoa taaluma hiyo ya plastic surgery kwa sasa.

Dk Mkoma alisema MNH inajivunia kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Australia akiwapo Daktari bingwa James Savundra ambaye ni Rais wa Madaktari Bingwa wa upasuaji kutoka timu ya upasuaji nchini Australia.

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Australia, Dk James Savundra alisema upasuaji huo ni moja ya upasuaji ambao umekuwa ukifanyika kwa gharama kubwa.

Post a Comment

0 Comments