Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
03 Novemba, 2016 amekutana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi
za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na kuzungumzia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini Tanzania yenye thamani ya
jumla ya Dola za Marekani Bilioni 1.6 zikiwa ni mkopo kutoka benki hiyo.
Akizungumza
baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Magufuli, Bi. Bella Bird
amesema mikopo hiyo inalenga kusaidia juhudi za maendeleo nchini
Tanzania na itatolewa katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati,
usafirishaji, elimu na maji.
"Miradi
hii yote imelenga zaidi kuharakisha maendeleo na kuleta matokeo katika
maisha ya Watanzania, ni miradi ambayo inahitaji uongozi na msukumo
mzuri kutoka Serikalini na tunafurahi kwamba Rais Magufuli ni kiongozi
ambaye ana dhamira ya dhati ya kusimamia maendeleo" amesema Bi. Bella Bird.
Kwa
upande wake Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea
kushirikiana na Tanzania katika maendeleo na ametoa wito kwa Benki hiyo
kuharakisha utoaji wa mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi.
"Tunataka
kuona mambo yanatokea badala ya kutumia muda mwingi kuzungumza, miradi
hii ina manufaa makubwa kwa watanzania na tungependa utekelezaji wake
ufanyike haraka, na ili ufanyike haraka Benki ya Dunia inapaswa
kutupatia mikopo kwa wakati unaofaa" amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amemhakikishia Bi. Bella Bird kuwa Serikali yake ya Awamu
ya Tano imejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa
sasa na itakayoanza kutekelezwa katika siku zijazo kwa mkopo kutoka
Benki ya Dunia.
Kwa
hivi sasa miradi 26 yenye thamani ya Jumla ya Dola za Marekani Bilioni
4.5 inatekelezwa hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
03 Novemba, 2016
0 Comments
on