Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta leo tarehe 01 Novemba, 2016 wamezindua barabara ya Southern By-pass iliyojengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi nchini Kenya.

Sherehe ya uzinduzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 28 na inayounganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi imefanyika katika eneo la Karen nje kidogo ya Jiji la Nairobi.

Akizungumza katika sherehe hiyo Rais Magufuli amempongeza Rais Kenyatta na Serikali yake kwa kujenga barabara hiyo ambayo sio tu itawasaidia wananchi wa Kenya bali pia itawasaidia wananchi wa Afrika Mashariki wanaotumia barabara zinazopitia Nairobi.

Rais Magufuli pia ameishukuru Serikali ya China kupitia benki yake ya Exim ambayo imetoa mkopo wa kujenga barabara hiyo, kwa kuendelea kuziamini nchi za Afrika Mashariki na kuzikopesha mikopo inayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.

“Wananchi wanahitaji maendeleo na haya ndio maendeleo, barabara hii itasaidia kuinua uchumi na itasaidia masuala ya kijamii” amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amesema viongozi wa Afrika Mashariki wameamua kufanya kazi ya kuharakisha maendeleo na kuinua maisha ya wananchi, na kwamba ili kufanikisha hilo wamedhamiria kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara zinazounganisha nchi wanachama na kujenga vituo vya pamoja vya utoaji wa huduma za mpakani (One Stop Border Post).

Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema kujengwa kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Nairobi na pia kutaboresha shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mhe. Kenyatta amemshukuru Rais Magufuli kwa kuungana nae kuzindua barabara hiyo na amesema Kenya itaongeza juhudi katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa barabara zinazounganisha Kenya na Tanzania zikiwemo barabara ya Malindi kupitia Saadani hadi Bagamoyo nchini Tanzania na barabara ya Voi – Taveta- Horiri-Arusha.

Sherehe za uzinduzi wa barabara ya Southern By-pass zimehudhuriwa na Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto.

Kabla ya kuzindua barabara hiyo Rais Magufuli ametembelea kiwanda kidogo cha kusindika maziwa cha Eldoville kilichopo katika eneo la Karen ambacho kinamilikiwa na familia ya mkulima Bw. James Karuga.

Familia hiyo ilianzisha kiwanda cha kusindika maziwa mwaka 1985 kwa uzalishaji wa chini ya lita 1,000 kwa siku na hivi sasa imefikia uzalishaji wa lita 5,000 kwa siku na inatarajia kuongeza uzalishaji hadi lita 70,000 katika mwaka mmoja ujao baada ya kuongeza kiwanda cha pili.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Nairobi
01 Novemba, 2016


==