Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob kwa tiketi ya CHADEMA ameshinda kiti cha Umeya wa Manispaa ya Ubungo baada ya kupata jumla ya kura 16 huku akimuacha mbali mpinzani wake wa CCM, Yusuph Yenga aliyepata kura 2.

Kwa upande wa Naibu Meya, Ramadhan Kwangaya aliyekuwa akigombea kwa tiketi ya CUF amepata kura 15 dhidi ya Kassim Lema wa CCM aliyepata kura 3.

Manispaa ya Ubungo imefanya uchaguzi wa kumchagua Meya na Naibu Meya jana kwa mara ya kwanza tangu Manispaa hiyo ilipoundwa kufuatia kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Ubungo ambapo ilipelekea kuvunjwa kwa Manispaa ya Kinondoni na kugawanywa.

Kabla Manispaa ya Kinondoni haijavunjwa na kuzaa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ndiye alikuwa Meya wa Manispaa hiyo.

Uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni ulifanyika juma lililopita ambapo wagombea wa CCM walishinda baada ya UKAWA kususia uchaguzi huo wakimtuhumu Mkurugenzi wa Manispaa kuongeza idadi ya wajumbe kinyemela ili waisaidie CCM kushinda.

Baada ya hapo UKAWA wamefungua kesi mahakamani wakiomba mahakama kufuta matokeo ya uchaguzi huo.


==