WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema  Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli imetoa  kipaumbele kikubwa katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Amesema hatua imejidhihirisha kwenye bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Serikali imetenga sh. trilioni 1.3 kwa ajili ya Sekta hiyo.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Ijumaa, Novemba 25,2016 kwenye harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya uboreshaji wa shule nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Saalam.

Akizungumza katika harambee hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Hassan Maajar Trust,  Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi kwamba bajeti ya Sekta ya elimu itaendelea kuongezeka kadri uwezo wa Serikali utakavyokuwa unaimarika.

“Kama mnavyofahamu, Serikali iliamua kuanza mara moja, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 ambayo inaelekeza Serikali kutoa elimu bure kwa watanzania wote kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari,” alisema.

Alisema uamuzi huo ulikuja na changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa madawati kufuatia ongezeko kubwa la wanafunzi waliodahiliwa.

Alisema kufuatia hali hiyo, tarehe 15 Machi, 2016 Serikali iliwaagiza Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha tatizo la madawati linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

“Napenda kuwaarifu kwamba, jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda kwani baadhi ya mikoa tayari imemaliza tatizo hilo kwa shule za msingi na sekondari, wakati Mikoa mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,”.

“Hadi sasa Mikoa ambayo imekamilisha zoezi hilo kwa shule za msingi na sekondari na kubaki na madawati ya ziada ni Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Mtwara, Njombe, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora,” alisema.

Waziri mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi na wananchi wa Mikoa hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika kumaliza kadhia hiyo kwa wanafunzi ambao walikuwa wanakaa chini. “Huo ndio uongozi tunaoutaka, uongozi wa kusimama bega kwa bega na wananchi na kutatua kero zao”,.

Wakati huo huo aliipongeza taasisi hiyo kwa kutoa mchango mkubwa katika kumaliza upungufu wa madawati katika baadhi ya Mikoa nchini  kupitia harambee mbalimbali.

Alisema kati ya mikoa 13 iliyopata ufadhili kutoka ya Taasisi ya Hassan Maajar Trust, mikoa 10 kati yake imefanikiwa kumaliza tatizo la madawati kwa shule zote za msingi na sekondari.

Mikoa hiyo ni pamoja na Njombe, Rukwa, Singida, Pwani, Shinyanga, Lindi, Mbeya, Iringa, Mtwara, na Kilimanjaro.

“Hii inathibitisha kwamba jitihada za pamoja kati ya Serikali na asasi zisizokuwa za Kiserikali zinaweza kuleta ufumbuzi wa changamoto nyingi zinazolikabili Taifa letu,”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa taasisi ya Hassan Maajar Trust Fund,    Balozi Mwanaidi Maajar, alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo miaka mitano iliyopita  imefanikiwa kuwainua watoto takribani 30,000 kutoka sakafuni kufuatia kampeni ya Dawati kwa Kila Mtoto