Huduma za kijamii na kiuchumi katikati ya jiji la Mwanza, hii leo zimesimama kwa siku nzima na kusababisha maelfu ya wakazi wa jiji hilo kukosa mahitaji muhimu yakiwemo ya vyakula kwenye migahawa,baada ya wafanyabiashara wa kati na wakubwa kufunga maduka yao kwa hofu ya kuibuka vurugu wakati mamia ya askari mgambo wa jiji hilo pamoja na Manispaa ya Ilemela walipokuwa wakiendesha operasheni safisha jiji.

Operesheni hiyo ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo katikati ya jiji la Mwanza pamoja na maeneo mengine ya halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilianza majira ya saa tano usiku wa kuamkia Jumamosi ikitekelezwa na askari mgambo zaidi ya 700, askari polisi na askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Mwanza.

Wakuu wa wilaya za Nyamagana na Ilemela;Mary Tesha na Dk.Leonard Masale wamekutana na waandishi wa habari na kuzungumzia zoezi hilo, waliloliita kuwa ni endelevu

Tofauti na operesheni ya kuwaondoa machinga katikati ya jiji la Mwanza iliyofanyika Desemba 15 mwaka 2013, ambapo polisi walionyoshewa vidole kwa matumizi ya silaha za moto na mabomu ya machozi yaliyosababisha baadhi ya machinga kupata ulemavu wa kudumu,safari hii mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mary Tesha anasema hapakuwa na matumizi ya nguvu kubwa.

Serikali imewaonya machinga hao kutojaribu kurejea katika maeneo waliyoondolewa ambayo ni Sahara,Makoroboi, Liberty na Stendi ya Tanganyika,kwani atakayekaidi agizo hilo atakumbana na nguvu za dola.