Baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kukwama tena kupata dhamana mahakamani jana, amewataka mawakili wake kutomhangaikia na kuliacha suala hilo kama lilivyo na atakaa gerezani hadi Januari mwakani.

 Akizungumza baada ya Mahakama Kuu kuondoa rufaa ya mbunge huyo aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumnyima dhamana, Wakili wa Lema, John Malya alisema mteja wake amewaomba kutokata tena rufaa na kuiachia Jamhuri iamue inavyotaka. 

“Baada ya kujadiliana na mbunge, tumeona tufuate kwanza maelekezo yake ya kutofanya lolote juu ya maombi mapya ya dhamana,” alisema Malya. 

Kutokana na maombi ya dhamana yake kukwama, Lema alirejeshwa kwenye Gereza la Kisongo ambako ataendelea kuwa mahabusi kusubiri hatima ya kesi inayomkabili. 

“Tulikuwa na njia nyingi za kufanya kwa ajili ya kudai haki ya dhamana ya Lema lakini mbunge ameshatoa agizo hilo,” alisema Malya. 

Aidha mke wa Lema, Neema Lema alisema amejadiliana na mumewe na kuona kinachoendelea kwenye shauri la kesi hiyo. 

“Wanasheria walitoa ushauri wa nini kifanyike lakini mume wangu ameamua kisifanyike chochote kuanzia sasa. Pamoja na yote yanayotokea sasa ifike mahala ieleweke kuwa nchi si mali ya mtu yeyote, bali ni mali ya Watanzania wote,” alisema Neema. 

Lema  alikamatwa Novemba 2, akiwa bungeni Dodoma na kurejeshwa Arusha kujibu mashtaka ya kutoa kauli za uchochezi namba 440 na 441/2016.

Katika kesi hiyo, anadaiwa kuwa kati ya Oktoba 23 na 26 alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli katika maeneo tofauti wakati wa mikutano yake ya hadhara. 

Tangu wakati huo mawakili wake wamejitahidi bila mafanikio kumtoa kwa dhamana na ndipo baadaye walikata rufaa Mahakama Kuu ambako pia imeshindikana kwa maelezo kuwa iliwasilishwa nje ya muda wa siku 10 unaotakiwa kisheria. 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angelo Rumisha akisoma uamuzi wa Jaji Mfawidhi, Fatuma Masengi alitaja sababu za kuondolewa rufaa hiyo kuwa ni mshtakiwa kushindwa kuonyesha kusudio la kukataa rufaa ndani ya muda. Pia, alisema Mahakama Kuu inafungwa mkono kutoa uamuzi mwingine. 

Rumisha alisema mshtakiwa alipaswa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa hiyo ndani ya siku 10, tangu uamuzi wa Mahakama ulipofanyika lakini badala yake upande wa utetezi ulikata rufaa nje ya siku 10. 

“Maamuzi yalifanyika tarehe 11 , ilipaswa hadi Novemba 21 wawe wameonyesha kusudio la kukata rufaa lakini walikata rufaa tarehe 22,”alisema Msajili. 

“Mahakama inaungana na pingamizi la Jamhuri, hivyo imeiondoa rufaa hii,”alisema. 

Awali, Jamhuri ndiyo iliweka pingamizi, kupitia mawakili wake, Paul Kadushi na Matenus Marandu ikipinga kusikilizwa kwa maombi ya rufaa hiyo ya Lema iliyowasilishwa na wakili Peter Kibatala kwa maelezo imekiuka sheria. 

Wakili Marandu alisema Kifungu cha Sheria 361 (1)(a) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinataka mkataji rufaa kuonyesha nia ya kukata rufaa kwa kuandika notisi ya rufaa hivyo kuitaka Mahakama itupilie mbali rufaa hiyo. 

Chadema wasikitika 
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisema kutokana na uamuzi huo, kwa sasa wanaheshimu uamuzi wa Lema kuiachia Jamhuri kuamua hatima yake. 

“Tumefedheheshwa sana na kitendo Msajili alichokifanya kuwa kama Lema ataongea mawakili wake watoke nje na kama haiwezekani asubiri mpaka pale atakapomaliza kusoma maamuzi,” alisema Amani 

Wakati Msajili akitaka kusoma uamuzi huo jana saa 3:50 asubuhi, Lema alinyoosha mkono akiashiria kutaka kuongea lakini hakupewa ruhusa na Msajili. Badala yake alisema mawakili wake ndiyo walipaswa kutoa hoja ya mshtakiwa huyo kwamba kama Lema ataongea itabidi mawakili wake watoke nje. 

Baada ya uamuzi kufanyika, Wakili wa Lema Adam Jabir alisimama na kutoa hoja ya mbunge huyo kumuomba Msajili awaruhusu ndugu zake mshtakiwa waingie ndani ya Mahakama kusikiliza shauri lake baada ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi. 

Msajili alijibu kuwa mahakama haina fedha za kununua vipaza sauti. Pia, alisema wamezuia watu wengine kuingia kwenye Mahakama hiyo kwa kuwa eneo hilo ni dogo. Lema amerudishwa mahabusu huku kukiwa na sintofahamu ya lini rufaa ya kupinga dhamana yake itasikilizwa.