Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wanachama watano wa Chadema pamoja na watu wengine watatu wasio raia wa Tanzania waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kimtandao.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washtakiwa hao jana chini ya Kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Waliachiwa huru, baada ya Wakili wa Serikali, Elia Athanas kuomba kufutwa kesi hiyo chini ya kifungu hicho na Mahakama kuridhia.

Kesi hiyo, imefutwa ikiwa katika hatua ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka baada ya kukamilisha upelelezi wao na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 27, 2015 na kusomewa mashtaka ya makosa ya uhalifu wa kimtandao, wakidaiwa kukusanya na kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Washtakiwa hao ni Mashinda Edwin Mtei, Julius Mwita, Fredrick Eddie Fussi, Meshack Carlos Mlawa na Anisa Nicholaus Rulanyaga.

Mbali na wanachama hao wa Chadema, washtakiwa wengine ambao ni raia wa kigeni ni Julius Mwonga Matei (Kenya), Jose Mavinga Nimi ambaye kwa sasa ni marehemu (Angola) na Kim Hyunwook (Korea) kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Uhalifu wa Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa pamoja, walidaiwa kuwa kati ya Oktoba 25 na 26, 2015 kwenye maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walichapisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2015 yasiyo sahihi na ambayo hayakuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa lengo la kuipotosha jamii.

Walidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, walichapisha na kusambaza matokeo hayo kupitia mfumo wa uratibu wa uchaguzi uitwao ‘M4C Election Results Management’ na kupitia mitandao mingine ya kijamii, kama vile Facebook na Twitter.

Washtakiwa Matei, Mavinga na Hyunwook wanadaiwa kujihusisha na ajira nchini bila ya kuwa na kibali, kinyume cha Sheria ya Uhamiaji. Wanadaiwa kuwa Oktoba 26, 2015 katika Hoteli ya King D, iliyoko wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wageni hao walijihusisha katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya uchaguzi wa urais nchini kwa Chadema bila kibali.

Pia wageni hao walidaiwa kujihusisha na shughuli za biashara nchini kwa niaba ya Wanama Saccos, bila ya kuwa na kibali kinyume cha Sheria ya Uhamiaji.