Mama mmoja anayejulikana kwa jina la Gaudensia Michael, mkazi wa Nyamakokoto Halmashauri ya Bunda, Mkoani Mara, amesema kuwa siku ya kwanza aliyomfuma mume wake kitandani na mwanaye, aliamua kusamehe kwa kuamini kuwa kitendo hicho cha baba kuwaingilia wanaye kisingeendelea tena.

Gaudensia ameyabainisha hayo , wakati mume wake akipelekwa katika kituo cha Polisi kilichopo wilayani humo kwa tuhuma za kuwabaka wanaye 2 kwa nyakati tofauti na huku mwanaye mwingine wa miaka 13 akimpa ujauzito, na kuiomba Serikali iingilie kati suala hilo kwa kuwa yeye hana jambo la kufanya tena.

"Kuna siku nilimkuta chumbani kitandani na mtoto, nikamuuliza nini kimekupungua mbona wanawake wengi sana, akaniambia mke wangu nisamehe, basi nikaachana na hilo suala kumbe likawa endelevu, mimi nakaa na wanangu kumbe ni wake wenzangu, kwa hili naomba Serikali inisaidie yamenitokea jamani na sina cha kufanya" amesimulia Mama wa watoto hao.

Yassin Ally ni Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la KIVULINI, amesema shule zitakapofunguliwa ni vyema wanafunzi wote wakapimwa ujauzito na magonjwa mengine, huku Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mji wa Bunda, Bonji Bugeni, akiitaka jamii kuwafichua wanaowafanyia vitendo vya ukatili watoto.