Header Ads Widget

Polisi Wamnyima Tundu Lissu Dhamana, Atupwa Rumande

JESHI la Polisi, kanda Maalumu ya Dar es Salaam
limemnyima dhamana, Tundu Lissu, Mwanasheria
Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), baada ya kumaliza kuhojiwa katika
kituo kikuu cha polisi.
Baadhi ya viongozi waliofika kumwekea dhamana
ni pamoja na Freeman Mbowe Mwenyekiti wa
Chadema, Edward Lowassa Waziri Mkuu wa
zamani na mjumbe wa kamati kuu wa Chama
hicho, aliyefika saa 12:14 jioni akiungana na
viongozi na wanachama wa chama hicho.
Baada ya kufika Lowassa wanachama na wafuasi
wa Chadema waliokuwa nje ya ofisi hizo za polisi
walianza kuimba wimbo wa kumuita rais, rais, rais
ikiwemo na kauli mbiu ya maarufu ya Peoles
power.
Mara baada ya kufika alipokelewa na Mwenyekiti
wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa
amepanda gari moja na Meya wa Kinondoni,
Boniface Jacob waliokuwa nje ya geti.
Viongozi hao waliokuwa nje baada ya kuzuiwa
kuingia ndani na polisi waliongozana na Lowassa
kuomba kuingia lakini walizuiwa hali iliyofanya
wachukue uamuzi wa kuondoka.
Kiongozi aliyeruhusiwa kuingia alikuwa ni Meya wa
Dar es Salaam, Isaya Mwita.
Akizungumzia kuhusu hilo, Peter Kibatala
mwanasheria wa Lissu alisema kwamba mahojiano
kati ya jeshi hilo na mtuhumiwa yalianza saa 9:30
hadi saa 12:30.
“Katika maelezo ya polisi wanasema kwamba
wakati Lissu akitoka mahakamani juzi kwenye kesi
yake alitamka maneno ya uchochezi, lakini haya
yote yanahitaji ushahidi,” alisema Kibatala.
Wakili huyo alisema kwamba polisi baada ya
kumaliza mahojiano na wao wakiwa wameandaa
utaratibu wa dhamana walikataliwa hadi leo Ijumaa
atakapofikishwa mahakamani.
Aliyesambaza Ujumbe Asakwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias
Sedoyeka ametangaza kumsaka mtu
aliyesambaza ujumbe ambao amaedai “una ishara
zote za uchochezi” unaoonyesha umeandikwa na
Lissu baada ya kukamatwa na jeshi hilo.
Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa
kina kwenye mitandao ya jamii kuhusu ujumbe
huo.
Ujumbe huo ambao pia umenukuliwa na jeshi hilo
katika taarifa yake, ulieleza jinsi polisi mkoani
Singida walivyomkamata Lissu baada ya kumaliza
mkutano wake wa hadhara huku akihamasisha
watu kutokubali kunyamazishwa na “Udikteta
Uchwara”.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina
kwenye mitandao ya jamii kuhusu ujumbe mfupi
wa maneno uliosambazwa katika mitandao hiyo
baada ya kukamatwa kwa Lissu ukiwa na ishara
zote za uchochezi…,” alisema Sedeyoka na
kuongeza:
“Katika uchunguzi huo endapo mtu yeyote
atabainika kutuma taarifa hiyo basi Jeshi la Polisi
halitasita kuchukua hatua kali za sheria
zinazostahili ikiwamo kumkamata na kuwafikisha
mahakamani mara moja.”
Ujumbe huo ulisomeka, “Wakubwa sana salamu.
Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini ya ulinzi
wa polisi Singida. Nimemaliza kuhutubia mkutano
wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao
makuu ya jimbo la Singida Mashariki.
“Mara baada ya kushuka jukwaani nilifuatwa na
RCO wa mkoa aliyejitambulisha kwa jina la Babu
Mollel na kuniarifu kuwa ameelezwa na RPC
nikamatwe. Wakati huohuo, kuna amri ya
kunikamata iliyotoka Dar es Salaam kwa hiyo nipo
nguvuni ninasubiri maelekezo ya wanapotaka
kunipeleka…
“Its likely (kuna uwezekano) nitasafirishwa Dar
usiku huu. Infact ni usiku huu kwa taarifa za sasa
hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa ‘there is no
turning back’ (hakuna kurudi nyuma), there is no
shutting up (hakuna kufunga mdomo). Nitapambana
kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote
nitakapokuwa.
“Whether in freedom or in jail as long as I have a
voice to speak with. (Nikiwa huru au kifungoni
ilimradi nina sauti ya kuzungumza) sitakubali
kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Msikubali
kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Aluta
continua!!!! From Tundu Lissu”.
Kamanda Sedoyeka alisema endapo itathibitishwa
kuwa Lissu ndiye aliyeandika na kusambaza
ujumbe huo ataingia tena matatani kwa
kukamatwa na kuchukuliwa hatua za sheria kama
lilivyoeleza jeshi hilo.
Hiyo ni mra ya tatu kukamtwa kwa mbunge huyo
kwa kipindi cha miezi michache na amekwisha
kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kwa tuhuma za uchochezi.
Kesi ya kwanza ni ile iliyodaiwa ametoa lugha ya
uchochezi katika habari iliyochapishwa na gazeti la
Mawio na kesi ya pili ni ya kutoa maneno ya
uchochezi kwa kumwita Rais Magufuli ‘Dikteta
Uchwara’

Post a Comment

0 Comments