Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuzuia
usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda
kuuchenjua nje ya nchi akitaka shughuli hizo
zifanyike nchini, imeelezwa kuwa utekelezaji wa
dhamira hiyo utachukua muda mrefu kutokana na
mchakato wake.
Juzi, Rais Magufuli alinukuliwa na vyombo vya
habari wilayani Kahama akisema katika uongozi
wake hataki kuona mchanga huo ukisafirishwa.
Alisema katika nchi zote zenye madini, Tanzania
ndiyo pekee inayosafirisha mchanga kwenda nje
hivyo akaagiza shughuli hiyo ifanyike nchini.
Agizo hilo limekuja wakati utafiti juu ya uwezekano
wa Tanzania kuwekeza katika mtambo wa
kuchenjua mchanga wa dhahabu ya uliofanywa na
Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA)
Februari 2011, ukionyesha kuwa ni uwekezaji
unaohitaji fedha nyingi.
Ripoti hiyo ilisema gharama za usimikaji mtambo
kamili wenye uwezo wa kuchenjua wastani wa tani
150,000 kwa mwaka, ingeweza kufikia Dola za
Marekani 500 milioni hadi Dola 800 milioni (sawa
na Sh1.1 trilioni hadi Sh1.74 trilioni za sasa).
Ripoti hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuangalia
uwezekano wa kuchenjua mchanga unaosafirishwa
na kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya
dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, ilieleza kuwa
baadhi ya mataifa yanayosafirisha mchanga huo
kwenda Japani na China ni Chile, Indonesia, Peru,
Marekani, Australia na Canada.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgodi wa Barrick (sasa
Accacia) huzalisha na kusafirisha kati ya tani
25,000 na 50,000 za mchanga huo kwa mwaka ili
kuchuja kiwango cha madini yaliyomo.
Akitoa maoni yake binafsi kuhusu agizo hilo,
Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika
alisema msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi
lakini utekelezaji wake utahitaji maandalizi
kutokana na ukubwa wa gharama za uwekezaji wa
mtambo huo.
Huku akisisitiza kuwa maoni hayo ni yake binafsi,
Mwanyika alisema ipo haja ya Serikali na sekta
binafsi kukaa pamoja kwa ajili ya kujadili shughuli
za uwekezaji huo hapa nchini.
“Nimemsikiliza Rais na nimemwelewa dhamira yake
lakini hajamaanisha amezuia rasmi, haiwezekani
kuzuia ghafla shughuli hizo. Pia sisi (wazalishaji) ni
tofauti kabisa na sekta hiyo ya uchenjuaji, kwa hiyo
itabidi kujadili nani awekeze, upatikanaji wa mikopo
itakuwaje na mambo mengi yanayohusiana,”
alisema.
Serikali iliwahi kulieleza Bunge wakati ikijibu swali
la aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli,
Aprili 2007 kuwa suala hilo ni la kisera kwa kuwa
wawekezaji wameruhusiwa na Serikali ilikwishajitoa
kwenye biashara.
Akijibu swali hilo ambalo Lembeli alitaka kujua
kwa nini mtambo huo usijengwe nchini, aliyekuwa
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence
Masha alisema hali hiyo imetokana na Serikali
kukosa wawekezaji au wawekezaji kuchelewa
kufanya hivyo hapa nchini.
Masha alilishauri Bunge lishirikiane na Serikali
kuendelea kuwakaribisha na kuwashawishi
wawekezaji kuja kuwekeza katika mtambo huo wa
kuchenjua mchanga, akibainisha kuwa uwekezaji
huo unahitaji mtaji mkubwa.
Miaka kadhaa iliyopita, aliyekuwa Mkurugenzi wa
Ukaguzi, Uzalishaji na Biashara ya Madini wa
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),
Liberatus Chizuzu alikaririwa akisema kuwa
gharama za uwekezaji wa mtambo huo ni kubwa
ikilinganishwa na thamani ya mapato
yanayopatikana kupitia uchenjuaji wa madini
yaliyopo.
Chizuzu alisema miongoni mwa masharti ya
uwekezaji wa mtambo huo ni upatikanaji wa
umeme wa uhakika, jambo ambalo ni changamoto
hapa nchini.
Angalizo la Lisu
Juzi, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
alitoa angalizo kuhusu hatua hiyo ya Rais akisema
Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao
wanalindwa kisheria na kimkataba.
Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alisema kwa
mujibu wa Sheria ya Madini na Mikataba ya
Uendelezaji Madini (MDA), madini yote
yanayochimbwa ni mali ya wawekezaji.
Alisema kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao
wanalindwa kisheria na kimkataba, hatua hiyo
inaweza kuwafanya wawekezaji hao kwenda
mahakama za usuluhishi za kimataifa.
Alisema Rais alitakiwa kufanya kama mwenzake,
Evo Morales wa Bolivia ambaye nchi yake ilikuwa
na mikataba kama ya Tanzania lakini
alipochaguliwa Desemba, 2006 aliiondoa kwanza
kwenye mikataba hiyo iliyokuwa inailazimisha
kuingia kwenye migogoro ya uwezekaji na baada
ya hapo ndipo akabadilisha sheria na mikataba ya
uwekezaji iliyoipa Bolivia sehemu kubwa ya
umilikaji wa gesi na mafuta ya nchi yake.
0 Comments
on