Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia
kuanza kutumia mitandao ya simu, kadi maalimu
na kadi za benki kwa ajili ya kulipia huduma za
matibabu ili kudhibiti changamoto za upotevu wa
fedha na wizi katika ukusanyaji wa mapato ya
hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma
kwa Wateja, Bw Aminiel Eligaesha, hospitali hiyo
imelenga pia kuimarisha njia za ukusanyaji mapato
ili kuboresha huduma za matibabu na kuboresha
maslahi kwa wafanyakazi.
Amesema mpango wa kutumia njia za kieletroniki
umelenga kukusanya mapato zaidi ili kuiwezesha
hospitali hiyo kukabiliana na changamoto
mbalimbali za uendeshaji na kutoa huduma bora
kwa wagonjwa.
Lengo la hospitali hiyo ni kuongeza mapato na
kupunguza matumizi na kutengeneza mazingira ya
kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wagonjwa
mbalimbali nchini.
“Hospitali imelenga kuboresha wadi za kulaza
wagonjwa wanaohitaji huduma na malazi binafsi,
kuhakikisha wagonjwa wanachangia huduma za
matibabu na kuboresha mfumo wa kuandaa hati za
madai kwa kampuni na mifuko ya Taifa ya bima ya
afya."
Taarifa hiyo imeeleza kwamba hospitali hiyo
imedhamiria pia kutoa motisha kwa wafanyakazi
wengine ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya
kazi.
Katika hatua nyingine, hospitali hiyo imeweka
mikakati ya kupunguza gharama za kununua dawa
na vifaa tiba kutoka viwandani (Manufacturers)
moja kwa moja.
“Kwa mfano, baada ya kupata kibali kutoka TFDA,
Hospitali imenunua dawa za figo
(immunosuppressant) kutoka India kwa Sh 226
milioni wakati hapa nchini zingegharimu Sh 500
milioni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, hospitali hiyo imeagiza nyuzi za kushonea
wagonjwa (sutures) kutoka kiwandani (Ethicon)
kwa gharama ya Sh 321 milioni wakati
zingegharimu Sh 668 milioni endapo
zingenunuliwa nchini.
Katika taarifa hiyo imebainisha kuwa hospitali hiyo
imeweza kupunguza gharama za uchujaji wa damu
(dialysis) kutoka wastani wa Sh 250,000 kwa kila
zamu (session) hadi kufikia Sh171,000.
0 Comments
on