Serikali ya Marekani, kupitia shirika lake la
Misaada ya Maendeleo USAID, imeipatia Tanzania
msaada wa dola Milioni 407 sawa na zaidi ya
shilingi Bilioni 895 zitakazotumika kwaajili ya
kuendeleza sekta za Kilimo, Afya, Nishati ya
Umeme, Elimu na Utawala Bora, katika kipindi cha
miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2016/2020.
Hati za makubaliano hayo zimetiwa saini Jijini Dar
es salaam, kati ya Mkurugenzi wa Shirika la USAID,
Bi. Sharon Cromer, na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile.
Msaada huo ni sehemu ya dola milioni 800, sawa
na zaidi ya shilingi trilion 1.76 ambazo serikali ya
Marekani kupitia USAID, imepanga kuipatia
Tanzania ili kufanikisha Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa katika kipindi cha miaka
mitano ijayo, wenye lengo la kuiwezesha Tanzania
kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda
ifikapo mwaka 2025.
Kiasi hicho cha fedha kitatumika na serikali ya
Tanzania kupitia mfuko mkuu moja kwa moja
wakati kiasi kingine kitatumiwa na Taasisi
zisizokuwa za kiserikali zinazofanya shughuli zake
hapa nchini kufanikisha malengo ya msaada huo.
Miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na
kupambana na UKIMWI na kifua kikuu, uzazi wa
mpango, kupunguza vifo vya mama na mtoto,
kukuza utawala wa kidemokrasia, usimamizi wa
rasilimali za taifa, na kuwekeza kwenye sekta ya
umeme ili kuimarisha sekta ya viwanda na
uzalishaji mali.
0 Comments
on