Wakati
leo ni mwaka mmoja tangu matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar yafutwe
Oktoba 28, 2015, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amemtuhumu
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha
kuwa ndiye aliikwamisha nchi kwa kupindua maamuzi ya wananchi.
Maalim Seif alisema kutokana na uamuzi huo, ndiyo maana mpaka sasa mwenyekiti huyo ameshindwa kuibuka hadharani akielewa alibeba dhima ya Wazanzibari na Watanzania wote wapenda amani.
Maalim
Seif aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika wilaya
zote saba za Unguja katika kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Jecha
alipofuta uchaguzi huo.
Maalim
Seif aliita siku hii ‘black October’ akisema ndiyo siku Jecha
alitekeleza kwa makusudi kufuta ndoto ya Wazanzibari ya kupata viongozi
wanaowataka.
“Jecha
ndiye aliyesitisha ndoto yetu ya kuwa Singapore, alipindua demokrasia
na kufuta matokeo bila ya kuwapo kifungu chochote cha Katiba kinachotoa
mamlaka hiyo,” alisema Maalim Seif.
Makamu
huyo wa kwanza wa Rais mstaafu, alisema kuwa kabla ya Jecha
hajatekeleza azma hiyo ovu, waangalizi wote wa uchaguzi kutoka ndani na
nje ya nchi na ZEC wenyewe walijiridhisha na kutoa tamko kuwa uchaguzi
ulikuwa huru na wa haki.
Waangalizi
hao ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Madola,
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC), Umoja
wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU).
“Nasema alichotekeleza Jecha ni dhuluma na mapinduzi ambayo yalilenga kupindua maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar,” alisisitiza Maalim Seif akiwahutubia viongozi na watendaji wa CUF wa wilaya za Unguja.
Alisema
yeye na viongozi wenzake wamekuwa wakiwatuliza wananchi na kwenda nao
bega kwa bega, wakielewa hakuna popote umma ulipodai haki yao duniani
kwa njia za kistaarabu na za kidemokrasia wakashindwa.
“Hivyo tambueni kuwa kimya kingi kina mshindo na haki yetu iliyoporwa haipo mbali kuipata kwani baada ya dhiki ni faraja,” alisema Maalim Seif.
“Jueni
kuwa katika kutekeleza hayo zipo njama za waziwazi za kutaka kuipitisha
Katiba ambayo haikupendekezwa na Watanzania kupitia maoni
yaliwasilishwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba,” alisema Maalim Seif.
Maalim
Seif alisema miongoni mwa njama hizo ni mazungumzo yanayoendelea sasa
kujaribu kuibua utaratibu wa kura ya maoni ili kuipitisha Katiba hiyo,
chini ya usimamizi wa ZEC na NEC.
Alisema
miongoni mwa njama za kuififisha Zanzibar ni mpango wa utafutaji na
uchimbaji wa mafuta na gesi na kuwakosesha wananchi fursa ya kufaidi
raslimali zao.
Jecha
hakupatikana jana kuzungunzia madai hayo, lakini Naibu katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipoulizwa alisema kwa sasa wapo katika
mkakati wa kuimarisha chama katika ngazi zote yakiwamo matawi yao.
“Unajua
sisi hatuzungumzii tena hayo, uchaguzi ulikwishafanyika na Serikali
ikaundwa na sasa inafanya kazi, la msingi tunaimarisha chetu,” alisema Vuai aliyeko katika ziara ya kichama kisiwani Pemba.
Akizungumza katika ofisi za CUF Wilaya ya Kati Unguja, Maalim Seif alisema, “Nataka
nikwambieni kilichotendeka kupitia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
hivi karibuni wakidai kujadili sheria ya uchimbaji mafuta, ni kiini
macho tu, maana hatujaona mabadiliko yoyote katika Katiba ya Jamhuri
tukielewa kwamba jambo hilo bado ni suala la Muungano.”
Maalim
Seif alihoji pia uhalali wa tamko la SMZ wa kumzuia asiongee na
wananchi misikitini, akisema hiyo ni katika njama za kumnyamazisha
asiyaeleze hayo.
Hivi
karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mohamed Aboud Mohamed alipiga marufuku hatua ya Maalim Seif kutembelea
na kuongea na wananchi misikitini.
Kufuatia hatua hiyo Maalim Seif alihoji akisema,
“Je, Mohamed Aboud haelewi wajibu wake, mbona hatujamsikia akikemea
uvunjwaji wa Katiba na pia ukiukwaji wa Sheria Na. 5 ya Vyama Vingi vya
Siasa ya Mwaka 1992, inayotoa ruhusa kufanya mikutano na maandamano,
hayaoni hayo, hajui kuwa yamepigwa marufuku kinyume na Katiba?”
KUTAZA..................MATOKEO........YADARASA......RA....SABA,
<<<<<<<<<BOFYA HAPA>>>>>>>>>>>>>>>>
<<<<<<<<<BOFYA HAPA>>>>>>>>>>>>>>>>
0 Comments
on